المزمل
The Enshrouded One • 20 ayahs • Meccan
بِسْمِ ٱللَّهِ ٱلرَّحْمَٰنِ ٱلرَّحِيمِ
1Ewe uliyejifunika!
2Kesha usiku kucha, ila kidogo tu!
3Nusu yake, au ipunguze kidogo.
4Au izidishe - na soma Qur-ani kwa utaratibu na utungo.
5Hakika Sisi tutakuteremshia kauli nzito.
6Hakika kuamka usiku kunawafikiana zaidi na moyo, na maneno yake yanatua zaidi.
7Kwani hakika mchana una shughuli nyingi.
8Na lidhukuru jina la Mola wako Mlezi, na ujitolee kwake kwa ukamilifu.
9Mola Mlezi wa mashariki na magharibi, hapana mungu isipokuwa Yeye, basi mfanye kuwa Mtegemewa wako.
10Na vumilia hayo wayasemayo, na jitenge nao kwa vizuri.
11Na niache Mimi na hao wanaokanusha, walioneemeka; na wape muhula kidogo!
12Hakika Sisi tunazo pingu nzito na Moto unaowaka kwa ukali kabisa!
13Na chakula kinachokwama kooni, na adhabu inayoumiza.
14Siku ambayo ardhi itatikiswa na milima pia, na milima itakuwa kama tifutifu la mchanga!
15Hakika Sisi tumemtuma kwenu Mtume aliye shahidi juu yenu, kama tulivyomtuma Mtume kwa Firauni.
16Lakini Firauni alimuasi huyo Mtume, basi tukamshika mshiko wa mateso.
17Basi nyinyi mkikufuru, mtawezaje kujikinga na Siku ambayo itawafanya watoto wadogo waote mvi?
18Hapo mbingu zitapasuka kwa sababu yake! Ahadi yake itakuwa imetekelezwa.
19Kwa hakika hili ni kumbusho. Mwenye kutaka atashika Njia ya kwendea kwa Mola wake Mlezi.
20Hakika Mola wako Mlezi anajua ya kuwa hakika wewe unakesha karibu na thuluthi mbili za usiku, na nusu yake, na thuluthi yake. Na baadhi ya watu walio pamoja nawe kadhalika. Na Mwenyezi Mungu ndiye anayeukadiria usiku na mchana. Anajua kuwa hamwezi kuweka hisabu, basi amekusameheni. Basi someni kilicho chepesi katika Qur-ani. Anajua ya kuwa baadhi yenu watakuwa wagonjwa, na wengine wanasafiri katika ardhi wakitafuta fadhila ya Mwenyezi Mungu, na wengine wanapigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo someni kilicho chepesi humo, na mshike Sala, na toeni Zaka, na mkopesheni Mwenyezi Mungu mkopo mwema. Na kheri yoyote mnayoitanguliza kwa ajili ya nafsi zenu mtaikuta kwa Mwenyezi Mungu, imekuwa bora zaidi, na ina thawabu kubwa sana. Na mtakeni msamaha Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.