الملك
The Sovereignty • 30 ayahs • Meccan
بِسْمِ ٱللَّهِ ٱلرَّحْمَٰنِ ٱلرَّحِيمِ
1Ametukuka ambaye mkononi mwake umo Ufalme wote; na Yeye ni Mwenye uwezo mno juu ya kila kitu.
2Ambaye ameumba mauti na uhai ili kukujaribuni ni nani miongoni mwenu mwenye vitendo vizuri zaidi. Na Yeye ni Mwenye nguvu, Mwenye msamaha mno.
3Aliyeumba mbingu saba kwa matabaka. Huoni tafauti yoyote katika uumbaji wa Mwingi wa Rehema. Hebu rudia kutazama! Je, unaona kosa lolote?
4Tena rudia kutazama mara mbili, kutazama kwako kutakurejelea mwenyewe hali ya kuwa kumehizika, kumechoka.
5Na kwa hakika tumeipamba mbingu ya chini kabisa kwa mataa, na tumeyafanya ili kuwapigia mashetani, na tumewaandalia adhabu ya Moto wenye mwako mkali.
6Na kwa wale waliomkufuru Mola wao Mlezi ipo adhabu ya Jahannamu. Na ni marejeo maovu yalioje hayo!
7Watakapotupwa humo, watausikia mngurumo wake na huku inafoka.
8Inakaribia kupasuka kwa hasira. Kila mara likitupwa kundi humo, walinzi wake huwauliza: 'Kwani hakukujieni mwonyaji?'
9Watasema: 'Kwani! Ametujia mwonyaji, lakini tulimkadhibisha, na tukasema: 'Mwenyezi Mungu hakuteremsha chochote. Nyinyi hamumo ila katika upotovu mkubwa!''
10Na watasema: 'Lau kuwa tungelisikia, au tungelikuwa tukitumia akili, tusingelikuwa katika watu wa Moto wenye mwako mkali!'
11Wakakiri dhambi zao. Basi kuangamia ni kwa watu wa Moto wenye mwako mkali!
12Hakika wale wanaomwogopa Mola wao Mlezi kwa ghaibu, watapata maghfira na ujira mkubwa.
13Na ficheni kauli zenu, au zidhihirisheni wazi; hakika Yeye anajua mno yaliyomo vifuani.
14Asijue yule aliyeumba, naye ndiye Mjua siri, Mwenye habari?
15Yeye ndiye aliyeidhalilisha ardhi kwa faida yenu, basi tembeeni katika pande zake, na kuleni katika riziki zake. Na kwake Yeye ndiyo kufufuliwa.
16Je, mmesalimika kutokana na aliyeko juu kuwa hatakudidimizeni kwenye ardhi, na tahamaki hiyo inatikisika!
17Au mnadhani mko salama kutokana na aliyeko juu ya kuwa Yeye hatakupelekeeni kimbunga chenye changarawe? Basi mtajua vipi maonyo yangu?
18Na bila ya shaka walikwisha kanusha wale waliokuwa kabla yao; basi kulikuwaje kukasirika kwangu?
19Kwani hawawaoni ndege walioko juu yao namna wanavyozikunjua mbawa zao, na kuzikunja? Hawashikilii ila Mwingi wa rehema. Hakika Yeye ni Mwenye kuona mno kila kitu.
20Au ni lipi hilo jeshi lenu la kukunusuruni badala ya Mwingi wa Rehema? Hakika makafiri hawamo ila katika udanganyifu.
21Au ni nani huyo ambaye atakupeni riziki kama Yeye akizuia riziki yake? Bali wao wanakakamia tu katika jeuri na kujiweka mbali.
22Je, anayekwenda akisinukia juu ya uso wake ni mwongofu zaidi, au yule anayekwenda sawasawa katika Njia iliyonyooka?
23Sema: Yeye ndiye aliyekuumbeni tangu mwanzo, na akakupeni uwezo wa kusikia na kuona na ufahamu wa nyoyo. Ni kidogo kabisa shukrani zenu.
24Sema: Yeye ndiye aliyekutawanyeni katika ardhi, na kwake mtakusanywa.
25Na wanasema: Lini ahadi hii, ikiwa mnasema ukweli?
26Sema: Hakika elimu ya hayo iko kwa Mwenyezi Mungu; na hakika mimi ni mwonyaji wa wazi tu mwenye kubainisha.
27Lakini watakapoiona karibu, nyuso za wale waliokufuru zitahuzunishwa, na itasemwa: Hayo ndiyo mliyokuwa mkiyaomba mno.
28Sema: Mwaonaje, ikiwa Mwenyezi Mungu ataniangamiza mimi na wale walio pamoja nami, au akiturehemu, ni nani atakayewalinda makafiri mbali na adhabu chungu?
29Sema: Yeye ndiye Mwingi wa Rehema; tunamuamini Yeye, na juu yake tunategemea. Basi mtakuja jua ni nani aliye katika upotovu ulio dhahiri.
30Sema: Mwaonaje, yakiwa maji yenu yamedidimia chini, ni nani atakuleteeni maji yanayomiminika?