يس
Ya-Sin • 83 ayahs • Meccan
بِسْمِ ٱللَّهِ ٱلرَّحْمَٰنِ ٱلرَّحِيمِ
1Ya Sin.[1]
2(Ninaapa) kwa Qur-ani yenye hekima!
3Hakika wewe ni miongoni mwa waliotumwa.
4Juu ya njia iliyonyooka.
5Uteremsho wa Mwenye nguvu, Mwingi wa kurehemu.
6Ili uwaonye watu ambao baba zao hawakuonywa, basi wao wamekuwa wenye kughafilika.
7Bila ya shaka kauli imekwisha thibiti juu ya wengi katika wao, kwa hivyo hawaamini.
8Tumeweka makongwa shingoni mwao, yakawafika videvuni. Kwa hivyo vichwa vyao viko juu tu.
9Tumeweka kizuizi mbele yao, na kizuizi nyuma yao. Na tumewafunika macho yao, kwa hivyo hawaoni.
10Ni sawa sawa kwao ukiwaonya au usiwaonye, hawataamini.
11Hakika wewe unamwonya mwenye kufuata ukumbusho, na akamcha Arrahman (Mwingi wa rehema), kwa ghaibu. Basi mbashirie huyo msamaha na ujira mwema.
12Hakika Sisi tunawafufua wafu na tunayaandika wanayoyatanguliza, na wanayoyaacha nyuma. Na kila kitu tumekihifadhi katika daftari la asili lenye kubainisha.
13Na wapigie mfano wa wakazi wa mji walipojiwa na Mitume.
14Tulipowatumia wawili, wakawakanusha. Basi tukawazidishia nguvu kwa mwingine wa tatu. Wakasema: "Hakika sisi tumetumwa kwenu."
15Wakasema: "Nyinyi si chochote ila ni watu kama sisi. Na Mwingi wa Rehema hakuteremsha kitu. Nyinyi mnasema uongo tu."
16Wakasema: "Mola wetu Mlezi anajua kwamba hakika sisi tumetumwa kwenu."
17Wala si juu yetu ila kufikisha ujumbe ulio wazi."
18Wakasema: "Sisi hakika sisi tunaona mkosi kwenu. Ikiwa hamtaacha basi kwa yakini tutakupigeni mawe, na mtapata adhabu chungu kutoka kwetu."
19Wakasema: "Mkosi wenu mnao wenyewe! Je! Ni kwa kuwa mnakumbushwa? Ama nyinyi ni watu waliopindukia mipaka."
20Na akaja mtu mbio kutokea upande wa mbali wa mjini, akasema: "Enyi watu wangu! Wafuateni hawa waliotumwa.
21Wafuateni ambao hawakutakini ujira, hali ya kuwa wenyewe wameongoka.
22Na kwa nini nisimuabudu yule aliyeniumba na kwake nitarejeshwa?
23Je, niishike miungu mingine badala yake? Arrahmani (Mwingi wa Rehema) akinitakia madhara uombezi wa hao hautanifaa kitu, wala hawataniokoa.
24Basi hakika mimi hapo nitakuwa katika upotovu ulio dhahiri.
25Hakika mimi nimemuamini Mola wenu Mlezi, basi nisikilizeni!"
26Akaambiwa: "Ingia Peponi!" Akasema: "Laiti kuwa watu wangu wangelijua.
27Jinsi Mola wangu Mlezi alivyonisamehe, na akanifanya miongoni mwa walioheshimiwa."
28Na hatukuwateremshia kaumu yake baada yake jeshi kutoka mbinguni, wala si wenye kuteremsha.
29Haukuwa ila ukelele mmoja tu, na mara walizimwa!
30Nawasikitikia waja wangu. Hawajii Mtume ila wao humkejeli.
31Je, hawaoni umma ngapi tulizoziangamiza kabla yao? Hakika hao hawarejei tena kwao.
32Na hapana mmoja ila wote watakusanywa waletwe mbele yetu.
33Na Ishara hiyo kwao ni ardhi iliyokufa, nasi tukaifufua, na tukatoa ndani yake nafaka, wakawa wanakula katika hizo!
34Na tukafanya ndani yake mabustani ya mitende na mizabibu, na tukatimbua chemichemi ndani yake.
35Ili wale katika matunda yake, na hayo hayakufanywa na mikono yao! Basi je, hawashukuru?
36Ametakasika yule aliyeumba dume na jike vyote katika vinavyomea katika ardhi na katika nafsi zao, na katika wasivyovijua.
37Na usiku ni Ishara kwao. Tunauvua humo mchana, mara wao wanakuwa gizani.
38Na jua linakwenda kwa kiwango chake. Hayo ni makadirio ya Mwenye nguvu, Mwenye kujua vyema.
39Na mwezi tumeupimia vituo, mpaka unakuwa kama karara kongwe.
40Haliwi jua kuufikia mwezi, wala usiku kuupita mchana. Na vyote vinaogelea katika njia zao.
41Na ni Ishara kwao kwamba Sisi tuliwapakia dhuria zao katika jahazi lililosheheni.
42Na tukawaumbia kutoka mfano wake wanavyovipanda.
43Na tukitaka, tunawazamisha, wala hapana wa kuwasaidia, wala hawaokolewi.
44Isipokuwa kwa rehema zitokazo kwetu na starehe kwa muda.
45Na wanapoambiwa: Jilindeni kutokana na yaliyoko mbele yenu na yaliyoko nyuma yenu, ili mpate kurehemewa...
46Na haiwafikii Ishara yoyote katika Ishara za Mola wao Mlezi isipokuwa wao huwa ni wenye kuipa mgongo.
47Na wanapoambiwa: "Toeni katika aliyokupeni Mwenyezi Mungu", wale waliokufuru huwaambia wale walioamini: Je, tuwalishe wale ambao Mwenyezi Mungu angependa angeliwalisha mwenyewe? Nyinyi hammo isipokuwa katika upotovu ulio dhahiri.
48Na wanasema: Ahadi hii itatokea lini, ikiwa nyinyi ni wakweli?
49Hawangojei isipokuwa ukelele mmoja tu utakaowachukua nao wamo kuzozana.
50Basi hawataweza kuusia, wala kwa watu wao hawarejei.
51Na litapulizwa baragumu, mara watatoka makaburini wakikimbilia kwa Mola wao Mlezi.
52Watasema: Ole wetu! Ni nani aliyetufufua kwenye malazi yetu? Haya ndiyo aliyoyaahidi Mwingi wa Rehema na wakasema kweli Mitume.
53Haitakuwa isipokuwa ukelele mmoja tu, mara wote watahudhurishwa mbele yetu.
54Basi leo nafsi yoyote haitadhulumiwa kitu, wala hamtalipwa isipokuwa yale mliyokuwa mkiyatenda.
55Hakika watu wa Bustani ya mbinguni leo wamo shughulini, wamefurahi.
56Wao na wake zao wamo katika vivuli wameegemea juu ya viti vya kifahari.
57Watapata humo kila namna ya matunda na watapata kila watakachokitaka.
58"Salama!" Hiyo ndiyo kauli itokayo kwa Mola Mlezi Mwenye kurehemu.
59Na enyi wakosefu! Jitengeni leo!
60Je, sikuagana nanyi, enyi wanadamu, kuwa msimuabudu Shetani? Hakika yeye ni adui dhahiri kwenu.
61Na ya kwamba mniabudu Mimi? Hii ndiyo Njia iliyonyooka.
62Na bila ya shaka yeye amekwisha lipoteza kundi kubwa miongoni mwenu. Je, hamkuwa mkifikiri?
63Hii basi ndiyo Jahannamu mliyokuwa mkiahidiwa.
64Ingieni humo leo kwa vile mlivyokuwa mkikufuru.
65Leo tunaviziba vinywa vyao, na iseme nasi mikono yao, na itoe ushahidi miguu yao kwa waliyokuwa wakiyachuma.
66Na tungelipenda, tungeliyafutilia mbali macho yao, wakawa wanaiwania njia. Lakini wangeionaje?
67Na tungelitaka, tungewageuza sura hapo hapo walipo, basi wasingeweza kwenda wala kurudi.
68Na tunayemzeesha, tunamrudisha nyuma katika umbo. Basi je, hawazingatii?
69Wala hatukumfundisha (Muhammad) mashairi, wala hayatakikani kwake hayo. Haukuwa huu isipokuwa ni ukumbusho na Qur-ani inayobainisha.
70Ili imwonye aliye hai, na neno litimie juu ya makafiri.
71Je, hawaoni kwamba tumewaumbia kutokana na iliyofanya mikono yetu wanyama wa mifugo, na wao wakawa wenye kuwamiliki.
72Na Sisi tukawadhalilishia. Basi baadhi yao wako wanaowapanda, na baadhi yao wanawala.
73Na wao wanapata kwao manufaa na vinywaji. Basi je, hawashukuru?
74Na wameishika miungu mingine badala ya Mwenyezi Mungu ili ati wapate kusaidiwa!
75Hawataweza kuwasaidia. Bali hao ndio askari wao, watahudhurishwa.
76Basi maneno yao yasikuhuzunishe. Hakika Sisi tunayajua wanayoyaweka siri na wanayoyadhihirisha.
77Kwani mwanadamu haoni ya kwamba Sisi tumemuumba yeye kutokana na tone la manii? Kisha sasa yeye ndiyo amekuwa ndiye mgomvi wa dhahiri!
78Na akatupigia mfano, na akasahau kuumbwa kwake, akasema: Ni nani huyo atakayeihuisha mifupa nayo imekwisha mung'unyika?
79Sema: Ataihuisha huyo huyo aliyeiumba hapo mara ya mwanzo. Na Yeye ni Mjuzi wa kila kuumba.
80Aliyekujaalieni kupata moto kutokana na mti wa kijani nanyi mkawa kwa huo mnawasha.
81Kwani aliyeziumba mbingu na ardhi hawezi kuwaumba mfano wao? Kwani! Naye ndiye Muumbaji Mkuu, Mjuzi mno.
82Hakika amri yake anapotaka kitu ni kukiambia tu: Kuwa! Na kikawa.
83Basi ametakasika yule ambaye mkononi mwake umo Ufalme wa kila kitu; na kwake Yeye mtarejeshwa.