الجن
The Jinn • 28 ayahs • Meccan
بِسْمِ ٱللَّهِ ٱلرَّحْمَٰنِ ٱلرَّحِيمِ
1Sema: Imefunuliwa kwangu ya kuwa kundi moja la majini lilisikiliza, na likasema: Hakika sisi tumeisikia Qur-ani ya ajabu!
2Inaongoza kwenye uongofu, kwa hivyo tumeiamini, wala hatutamshirikisha yeyote na Mola wetu Mlezi.
3Na kwa hakika utukufu wa Mola wetu Mlezi umetukuka kabisa; hana mke wala mwana.
4Na kwa hakika wapumbavu miongoni mwetu walikuwa wakisema uongo uliopindukia mipaka juu ya Mwenyezi Mungu.
5Nasi tulidhani kuwa watu na majini hawamzulii uongo Mwenyezi Mungu.
6Na hakika walikuwako wanaume katika watu waliokuwa wakitafuta kujikinga kwa wanaume wa kijini; kwa hivyo wakawazidisha madhambi.
7Na kwa hakika wao walidhani, kama mlivyodhani nyinyi, ya kuwa Mwenyezi Mungu hatamleta Mtume.
8Nasi tulifanya bidii kufika kwenye mbingu, lakini tukazikuta zimejaa walinzi wenye nguvu na vimondo.
9Na hakika tulikuwa tukikaa humo katika baadhi ya makao ili kusikiliza; lakini sasa anayetaka kusikiliza atakuta kimondo kinamvizia!
10Nasi hatujui kama wanatakiwa shari wale wanaokaa kwenye ardhi au Mola wao Mlezi anawatakia uongofu.
11Na hakika katika sisi wamo walio wema, na wengine wetu ni kinyume na hivyo. Tumekuwa njia mbali mbali.
12Nasi tulijua kuwa hatutomshinda Mwenyezi Mungu duniani, wala hatuwezi kumponyoka kwa kukimbia.
13Nasi tulipousikia uongofu tuliuamini. Basi mwenye kumuamini Mola wake Mlezi basi haogopi kupunjwa wala kudhulumiwa.
14Na hakika wamo katika sisi Waislamu, na wamo kati yetu wanaoacha haki. Basi waliosilimu, hao ndio waliotafuta uongofu.
15Na ama wanaoacha haki, hao watakuwa kuni za Jahannamu.
16Na lau kama wangelisimama sawasawa juu ya njia tungeliwanywesha maji kwa wingi.
17Ili tuwajaribu kwa hayo. Na anayepuuza kumkumbuka Mola wake Mlezi atamsukuma kwenye adhabu ngumu.
18Na hakika misikiti ni ya Mwenyezi Mungu, basi msimuabudu yeyote pamoja na Mwenyezi Mungu.
19Na hakika Mja wa Mwenyezi Mungu aliposimama kumwomba, wao walikuwa karibu kumzonga!
20Sema: Hakika mimi namwomba Mola wangu Mlezi, wala simshirikishi Yeye na yeyote.
21Sema: Mimi sina mamlaka ya kukudhuruni wala kukuongozeni.
22Sema: Hakika hapana yeyote awezaye kunilinda na Mwenyezi Mungu, wala sitapata pa kukimbilia isipokuwa kwake Yeye tu.
23Ila nifikishe Ujumbe utokao kwa Mwenyezi Mungu na risala zake. Na wenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi hakika hao watapata Moto wa Jahannamu wadumu humo milele.
24Hata watakapo yaona wanayoahidiwa, ndipo watakapojua ni nani mwenye msaidizi dhaifu, na mchache wa idadi.
25Sema: Sijui kama yapo karibu hayo mnayoahidiwa, au Mola wangu Mlezi atayawekea muda mrefu.
26Yeye ndiye Mwenye kujua ya siri, wala hamdhihirishii yeyote ghaibu yake.
27Isipokuwa Mtume wake aliyemridhia. Naye huyo humwekea walinzi mbele yake na nyuma yake.
28Ili Yeye ajue kwamba wao wamefikisha ujumbe wa Mola wao Mlezi, na Yeye anayajua vyema yote waliyo nayo, na amedhibiti idadi ya kila kitu.