نوح
Noah • 28 ayahs • Meccan
بِسْمِ ٱللَّهِ ٱلرَّحْمَٰنِ ٱلرَّحِيمِ
1Hakika Sisi tulimtuma Nuhu kwa watu wake: Kwamba waonye kaumu yako kabla ya kuwafikia adhabu chungu.
2Akasema: Enyi watu wangu! Kwa hakika mimi ni mwonyaji wa dhahiri kwenu.
3Ya kwamba mumuabudu Mwenyezi Mungu, na mumche Yeye, na mumtii.
4Atakughufirieni madhambi yenu, na atakuakhirisheni mpaka muda uliowekwa. Hakika muda wa Mwenyezi Mungu utapofika haucheleweshwi. Laiti mngejua!
5Akasema: Ee Mola wangu Mlezi! Hakika mimi nimewaita watu wangu usiku na mchana.
6Lakini wito wangu haukuwazidisha ila kukimbia.
7Na hakika mimi kila nilipowaita ili upate kuwaghufiria, walijiziba masikio yao kwa vidole vyao, na wakajigubika nguo zao, na wakakamia, na wakatakabari vikubwa mno!
8Tena niliwaita kwa uwazi.
9Kisha nikawatangazia hadharani, tena nikasema nao kwa siri.
10Nikasema: Ombeni msamaha kwa Mola wenu Mlezi; hakika Yeye ni Mwingi wa kusamehe.
11Atakuleteeni mvua inyeshe mfululizo.
12Na atakupeni mali na wana, na atakupeni mabustani na atakufanyieni mito.
13Mna nini hamweki heshima ya Mwenyezi Mungu?
14Na hali Yeye kakuumbeni daraja baada ya daraja?
15Kwani hamwoni jinsi Mwenyezi Mungu alivyoziumba mbingu saba kwa matabaka?
16Na akaufanya mwezi ndani yake uwe nuru, na akalifanya jua kuwa taa?
17Na Mwenyezi Mungu amekuotesheni katika ardhi kama mimea.
18Kisha atakurudisheni humo na atakutoeni tena.
19Na Mwenyezi Mungu amekukunjulieni ardhi kama busati.
20Ili mtembee humo katika njia zilizo pana.
21Nuhu akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika hao wameniasi, na wamemfuata yule ambaye mali yake na wanawe hawakumzidishia ila hasara.
22Na wakapanga vitimbi vikubwa.
23Na wakasema: Kamwe msiiache miungu yenu, wala msimwache Wadda wala Suwaa' wala Yaghutha, wala Yau'qa, wala Nasra.
24Na hao walikwisha wapoteza wengi, wala usiwazidishie waliodhulumu ila kupotea.
25Basi kwa ajili ya makosa yao waligharikishwa wakaingizwa Motoni, wala hawakuwapata wa kuwanusuru badala ya Mwenyezi Mungu.
26Na Nuhu akasema: Mola wangu Mlezi! Usimwache juu ya ardhi mkazi wake yeyote katika makafiri!
27Hakika ukiwaacha watawapoteza waja wako, wala wao hawatazaa ila waovu makafiri.
28Mola wangu Mlezi! Nighufirie mimi na wazazi wangu, na kila aliyeingia nyumbani mwangu kuwa ni mwenye kuamini, na Waumini wote wanaume, na Waumini wanawake. Na wala usiwazidishie waliodhulumu ila kupotea.