المعارج
The Ascending Stairways • 44 ayahs • Meccan
بِسْمِ ٱللَّهِ ٱلرَّحْمَٰنِ ٱلرَّحِيمِ
1Muulizaji aliuliza juu ya adhabu itakayotokea.
2Kwa makafiri - ambayo hapana awezaye kuizuia.
3Kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mwenye mbingu za daraja.
4Malaika na Roho hupanda kwenda kwake katika siku ambayo kiasi chake ni miaka hamsini elfu!
5Basi subiri kwa subira njema.
6Hakika wao wanaiona iko mbali.
7Na Sisi tunaiona iko karibu.
8Siku ambayo mbingu zitakapokuwa kama madini iliyoyeyushwa.
9Na milima itakuwa kama sufi.
10Wala jamaa hatamuuliza jamaa yake.
11Ijapokuwa wataonyeshwa waonane. Atatamani mkosefu lau ajikomboe na adhabu ya siku hiyo kwa kuwatoa fidia wanawe.
12Na mkewe, na nduguye.
13Na jamaa zake waliokuwa wakimkimu,
14Na wote waliomo duniani, kisha aokoke yeye.
15La, hasha! Kwa hakika huo ni Moto mkali kabisa,
16Unaobambua ngozi ya kichwa!
17Utamwita kila aliyegeuza mgongo na akageuka.
18Na akakusanya mali, kisha akayahifadhi.
19Hakika mtu ameumbwa na papara.
20Inapomgusa shari hupapatika.
21Na inapomgusa kheri huizuilia.
22Isipokuwa wanaosali.
23Ambao wanadumisha Sala zao.
24Na ambao katika mali yao iko haki maalumu.
25Kwa mwenye kuomba na anayejizuilia kuomba;
26Na ambao wanaisadiki Siku ya Malipo.
27Na ambao wanaiogopa adhabu itokayo kwa Mola wao Mlezi.
28Hakika adhabu ya Mola wao Mlezi si ya kuwa na amani nayo.
29Na ambao wanahifadhi tupu zao.
30Isipokuwa kwa wake zao, au iliyowamiliki mikono yao ya kuume, basi hao hawalaumiwi.
31Lakini wanaotaka kinyume cha haya, basi hao ndio wanaoruka mipaka.
32Na ambao wanazichunga amana zao na ahadi zao,
33Na ambao wanasimama imara katika ushahidi wao,
34Na ambao wanazihifadhi Sala zao.
35Hao ndio watakaoheshimiwa katika Bustani ya mbinguni.
36Wana nini wale waliokufuru wanakutumbulia macho tu?
37Makundi kwa makundi upande wa kulia na upande wa kushoto!
38Kwani kila mmoja wao anatumai kuingizwa katika Bustani ya mbinguni ya neema?
39La, hasha! Hakika Sisi tumewaumba kutokana na wanachokijua.
40Basi naapa kwa Mola Mlezi wa mashariki zote na magharibi zote kwamba Sisi tunaweza.
41Kuwabadili kwa walio bora kuliko wao; na Sisi hatushindwi.
42Basi waache wapige porojo na wacheze, mpaka wakutane na siku yao wanayoahidiwa.
43Siku watakapotoka makaburini kwa upesi kama kwamba wanakimbilia mfundo.
44Macho yao yatainama, fedheha itawafunika. Hiyo ndiyo Siku waliyokuwa wakiahidiwa.