الحجر
The Rocky Tract • 99 ayahs • Meccan
بِسْمِ ٱللَّهِ ٱلرَّحْمَٰنِ ٱلرَّحِيمِ
1Alif Lam Ra.[1] Hizi ni Aya za Kitabu na Qur-ani inayobainisha.
2Huenda ikawa wale waliokufuru wakatamani kwamba wangekuwa Waislamu.
3Waache wale, na wastarehe, na yawazuge matumaini. Basi watakujajua.
4Na hatukuuangamiza mji wowote ule isipokuwa ulikuwa na muda wake maalumu ulioandikiwa.
5Hawawezi umma wowote kuutangulia muda wao, wala kuchelewa.
6Na walisema, "Ewe uliyeteremshiwa Ukumbusho! Hakika wewe ni mwendawazimu.
7Mbona hutuletei Malaika ikiwa wewe ni miongoni mwa wakweli?"
8Sisi hatuwateremshi Malaika isipokuwa kwa sababu ya haki, na hapo hawatapewa muhula.
9Hakika Sisi ndio tuliouteremsha Ukumbusho huu, na hakika Sisi ndio tutakaoulinda.
10Na hakika tulikwishatuma Mitume kabla yako kwa mataifa ya mwanzo.
11Na hakuwajia Mtume yeyote isipokuwa walikuwa wakimfanyia stihizai.
12Na kama hivi ndivyo tunavyoyaingiza katika nyoyo za wahalifu.
13Hawayaamini haya, na ilhali imekwishawapitia desturi ya wa mwanzo.
14Na lau tungeliwafungulia mlango huko mbinguni, wakawa wanapanda kupitia humo,
15Basi wangelisema: Hakika macho yetu yameleweshwa tu. Bali sisi wenyewe ni kaumu tuliofanyiwa uchawi.
16Na hakika tumeweka katika mbingu vituo vya sayari, na tumezipamba kwa wenye kuangalia.
17Na tumezilinda kutokana na kila shetani aliyelaaniwa.
18Isipokuwa mwenye kusikiliza kwa kuibia, naye hufuatwa na kijinga cha moto kilicho dhahiri.
19Na ardhi tumeitandaza, na humo tumeweka milima madhubuti, na tumeotesha ndani yake katika kila kitu kwa kiasi chake.
20Na tumewafanyia humo vitu vya maisha yenu, na ya hao ambao nyinyi sio wenye kuwaruzuku.
21Na hakuna chochote ila asili yake inatokana na Sisi; wala hatukiteremshi isipokuwa kwa kipimo maalumu.
22Na tunazipeleka pepo za kupandishia, na tunateremsha kutoka mbinguni maji, kisha tukakunywesheni maji hayo. Wala si nyinyi mnayoyaweka.
23Na hakika Sisi ndio tunaohuisha na tunaofisha. Na Sisi ndio Warithi.
24Na hakika tunawajua waliotangulia katika nyinyi, na tunawajua waliobaki nyuma.
25Na hakika Mola wako Mlezi ndiye atakayewakusanya. Hakika Yeye ni Mwenye hekima, Mwenye kujua mno.
26Na hakika tulimuumba Mtu kwa udongo unaotoa sauti, unaotokana na matope yaliyotiwa sura.
27Naye Jini tulimuumba hapo kabla kutokana na moto wa upepo umoto.
28Na Mola wako Mlezi alipowaambia Malaika: Hakika Mimi nitamuumba mtu kwa udongo unaotoa sauti, unaotokana na matope yaliyotiwa sura.
29Basi nitakapomtengeneza sawasawa, na nikampulizia katika roho yangu, basi angukeni kumsujudia.
30Basi Malaika wote pamoja walimsujudia.
31Isipokuwa Iblisi. Yeye alikataa kuwa pamoja na waliosujudu.
32(Mwenyezi Mungu) akasema: Ewe Iblisi! Una nini hata hukuwa pamoja na waliosujudu?
33Akasema: Haiwi mimi nimsujudie mtu uliyemuumba kutokana na udongo unaotoa sauti, unaotokana na matope yaliyotiwa sura.
34(Mwenyezi Mungu) akasema: Basi toka humo, kwani hakika wewe umefukuziliwa mbali!
35Na hakika juu yako ipo laana mpaka Siku ya Malipo.
36Akasema (Iblisi): Mola wangu Mlezi! Nipe muhula mpaka siku watakapofufuliwa.
37(Mwenyezi Mungu) akasema: Hakika wewe ni katika waliopewa muhula.
38Mpaka siku ya wakati maalumu.
39Akasema: Mola wangu Mlezi! Ilivyokuwa umenipoteza, basi hakika nitawapambia katika dunia na hakika nitawapoteza wote.
40Isipokuwa waja wako walioteuliwa miongoni mwao.
41Akasema: Hii ni njia ya kujia kwangu iliyonyooka.
42Hakika waja wangu, wewe hutakuwa na mamlaka juu yao, isipokuwa wale watakaokufuata miongoni mwa wapotovu.
43Na hakika Jahannamu ndipo mahali pao walipoahidiwa wote.
44Ina milango saba; kila mlango ulitengewa sehemu miongoni mwao.
45Hakika wacha Mungu watakuwa katika Mabustani na chemchemi.
46(Wataambiwa:) Ingieni humo kwa salama na amani.
47Na tutaondoa chuki iliyokuwa vifuani mwao, wawe ndugu, juu ya viti vya kifahari huku wameelekeana.
48Humo hayatawagusa machovu, wala hawatatolewa humo.
49Wape habari waja wangu ya kwamba Mimi ndiye Mwenye kusamehe zaidi, Mwingi wa kurehemu.
50Na kwamba adhabu yangu ndiyo adhabu iliyo chungu!
51Na wape habari za wageni wa Ibrahim.
52Walipoingia kwake na wakasema: Salama! Yeye akasema: Hakika sisi tunawaogopa.
53Wakasema: Usiogope. Hakika, Sisi tunakubashiria kijana mwenye elimu mno.
54Akasema: Mnanibashiria nami uzee umenishika! Basi ni kwa njia gani mnanibashiria?
55Wakasema: Tunakubashiria kwa haki, basi usiwe miongoni mwa wanaokata tamaa.
56Akasema: Na ni nani anayekata tamaa na rehema ya Mola wake Mlezi isipokuwa wapotovu?
57Akasema: Hebu mna jambo gani, enyi wajumbe?
58Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwa kaumu ya wahalifu!
59Isipokuwa watu wa familia ya Lut'. Bila ya shaka sisi tutawaokoa hao wote.
60Isipokuwa mkewe. Tumekwishapitisha kwamba huyo hakika atakuwa miongoni mwa watakaosalia nyuma.
61Basi wajumbe hao walipowajia watu wa familia ya Lut'.
62(Lut') Alisema: Hakika nyinyi ni kaumu msiojulikana.
63Wakasema: Bali sisi tumekuletea yale waliyokuwa wakiyafanyia shaka.
64Na tumekujia kwa Haki, na hakika sisi ni wakweli.
65Basi ondoka na ahali zako usiku ungalipo, nawe ufuate nyuma yao, wala yeyote kati yenu asigeuke nyuma. Na mwende huko mnakoamrishwa.
66Na tukamfunulia hukumu hiyo, ya kwamba hata wa mwisho wao hao ikifika asubuhi atakuwa amekwishakatiliwa mbali.
67Na wakaja watu wa mji huo huku wamefurahi mno.
68Akasema: Hakika hawa ni wageni wangu. Basi msinifedheheshe.
69Na mcheni Mwenyezi Mungu, wala msinihizi.
70Wakasema: Kwani hatukukukataza (kuwakaribisha) walimwengu hawa?
71Akasema, "Hawa binti zangu (waoeni)[1], ikiwa nyinyi ni watendaji."
72Ninaapa kwa uhai wako! Hakika hao walikuwa katika ulevi wao, wakihangaika ovyo.
73Basi ukelele ukawatwaa wakipambaukiwa.
74Kwa hivyo, tukaugeuza mji huo juu chini, na tukawanyeshea mvua ya mawe ya udongo wa kutoka Motoni.
75Hakika katika hayo zipo ishara kwa wanaotafakari na kuzingatia.
76Na hakika miji hii ipo kwenye njia wazi inayopitiwa.
77Hakika katika hayo ipo ishara kwa Waumini.
78Na hakika watu wa Kichakani walikuwa madhalimu.
79Kwa hivyo tukawaadhibu. Na hakika miji miwili hii iko kwenye njia iliyo wazi.
80Na bila ya shaka wakazi wa Hijr waliwakadhibisha Mitume.
81Na tuliwaletea ishara zetu, nao wakawa wanazipa migongo.
82Nao walikuwa wakichonga majumba katika milima kwa amani.
83Basi ukelele ukawatwaa asubuhi.
84Na hayakuwafaa yale waliyokuwa wakiyachuma.
85Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyo kati yake isipokuwa kwa haki. Na hakika Saa ya Kiyama itafika. Basi samehe msamaha mzuri.
86Hakika Mola wako Mlezi ndiye Muumbaji, Mwenye kujua zaidi.
87Na hakika tumekupa (aya) saba zinazosomwa mara kwa mara, na Qur-ani Tukufu.
88Kamwe usivinyoshee macho yako vitu tulivyowastarehesha kwavyo makundi fulani kati yao, wala usiwahuzunikie. Na wainamishie bawa lako (la huruma) Waumini.
89Na sema: Hakika mimi ndiye mwonyaji mwenye kubainisha.
90Kama hivyo tuliwateremshia waliogawa.
91Ambao waliifanya Qur-ani vipande vipande.
92Basi ninaapa kwa Mola wako Mlezi! Lazima tutawauliza wote.
93Kuhusu yale waliyokuwa wakiyatenda.
94Basi wewe yadhihirishe yale uliyoamrishwa, na jitenge mbali na washirikina.
95Hakika Sisi tunatosha kukukinga kutokana na wanaofanya stihizai.
96Ambao wanafanya mungu mwingine kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu. Basi watakujajua!
97Na Sisi tunajua kwa hakika kuwa wewe kifua chako kinaona dhiki kwa hayo wayasemayo.
98Basi mtakase Mola wako Mlezi kwa kumsifu, na uwe miongoni mwa wanaomsujudia.
99Na muabudu Mola wako Mlezi mpaka ikufikie Yakini.