المدثر
The Cloaked One • 56 ayahs • Meccan
بِسْمِ ٱللَّهِ ٱلرَّحْمَٰنِ ٱلرَّحِيمِ
1Ewe uliyejigubika!
2Simama uonye!
3Na Mola wako Mlezi mtukuze!
4Na nguo zako, zisafishe.
5Na yaliyo machafu yahame!
6Wala usitoe kwa kutaraji kuzidishiwa.
7Na kwa ajili ya Mola wako Mlezi, subiri!
8Basi litakapopulizwa baragumu.
9Siku hiyo, basi, itakuwa siku ngumu.
10Kwa makafiri haitakuwa nyepesi.
11Niache peke yangu na niliyemuumba.
12Na nikamjaalia awe na mali mengi.
13Na wana wanaoonekana.
14Na nikamtegenezea mambo vizuri kabisa.
15Kisha anatumai nimzidishie!
16Hasha! Kwani hakika yeye alikuwa akizifanyia ukaidi Aya zetu!
17Nitamtesa kwa mateso yasiowezekana.
18Kwani hakika yeye alifikiri na akapima.
19Basi ameangamia! Vipi alivyopima!
20Tena ameangamia! Vipi alivyopima!
21Kisha akatazama.
22Kisha akakunja kipaji, na akanuna.
23Kisha akaipa kisogo haki, na akatakabari.
24Na akasema: Haya si chochote ila ni uchawi ulionukuliwa.
25Haya si chochote ila kauli ya binadamu.
26Nitakuja mtia kwenye Moto wa Saqar.
27Na nini kitakujuulisha ni nini huo Moto wa Saqar?
28Haubakishi wala hausazi.
29Unababua ngozi iwe nyeusi.
30Juu yake wapo kumi na tisa.
31Na hatukuwafanya walinzi wa Motoni ila ni Malaika, wala hatukuifanya idadi yao hiyo ila kuwatatanisha waliokufuru, wapate kuwa na yakini waliopewa Kitabu, na wazidi Imani wale walioamini, wala wasiwe na shaka waliopewa Kitabu na Waumini, na wapate kusema wenye maradhi katika nyoyo zao na makafiri: "Mwenyezi Mungu amekusudia nini kwa mfano huu?" Ndiyo kama hivyo Mwenyezi Mungu humwacha apotee amtakaye, na humwongoa amtakaye. Na hapana yeyote anayejua majeshi ya Mola wako Mlezi ila Yeye tu. Na haya si chochote ila ni ukumbusho kwa binadamu.
32Hasha! Naapa kwa mwezi!
33Na kwa usiku unapokucha!
34Na kwa asubuhi inapopambazuka!
35Hakika huo Moto ni katika mambo yaliyo makubwa kabisa!
36Ni onyo kwa binaadamu.
37Kwa anayetaka miongoni mwenu kutangulia au kuchelewa.
38Kila nafsi imo rahanini kwa mabaya iliyoyachuma.
39Isipokuwa watu wa kuliani.
40Hao watakuwa katika Mabustani, wawe wanaulizana
41Habari za wakosefu:
42Ni nini kilichokupelekeni Motoni?
43Waseme: Hatukuwa miongoni mwa waliokuwa wakisali.
44Wala hatukuwa tukiwalisha masikini.
45Na tulikuwa tukizama pamoja na waliozama katika maovu.
46Na tulikuwa tukiikanusha Siku ya Malipo.
47Mpaka yakini (yaani mauti) ilipotufikia.
48Basi hautawafaa kitu uombezi wa waombezi.
49Basi wana nini hata wanapuuza onyo hili?
50Kana kwamba wao ni mapunda waliotimuliwa.
51Wanaomkimbia simba!
52Ati kila mmoja katika wao anataka apewe nyaraka zilizofunuliwa.
53Hasha! Kwani wao hawaiogopi Akhera?
54Hasha! Kwa hakika huu ni ukumbusho!
55Basi anayetaka atakumbuka.
56Na hawatakumbuka isipokuwa Mwenyezi Mungu atake. Ucha Mungu ni kwake Yeye, na msamaha ni wake Yeye.