القيامة
The Resurrection • 40 ayahs • Meccan
بِسْمِ ٱللَّهِ ٱلرَّحْمَٰنِ ٱلرَّحِيمِ
1Ninaapa kwa Siku ya Kiyama!
2Na ninaapa kwa nafsi inayojilaumu!
3Anadhani mtu kuwa Sisi hatutaikusanya mifupa yake?
4Kwani! Sisi tunaweza hata kuziweka sawa sawa ncha za vidole vyake!
5Lakini mtu anataka tu kuendelea na maasi kwa siku zilizoko mbele yake.
6Anauliza: Lini itakuwa hiyo Siku ya Kiyama?
7Basi jicho litakapodawaa,
8Na mwezi utakapopatwa,
9Na likakusanywa jua na mwezi,
10Siku hiyo mtu atasema: Yako wapi makimbilio?
11La! Hapana pa kukimbilia!
12Siku hiyo pa kutua ni kwa Mola wako Mlezi tu.
13Siku hiyo ataambiwa aliyoyatanguliza na aliyoyaakhirisha.
14Bali mtu ni hoja juu ya nafsi yake.
15Na ingawa atatoa chungu ya udhuru.
16Usiutikisie huu wahyi ulimi wako kwa kuufanyia haraka.
17Hakika ni juu yetu kuukusanya na kuusomesha.
18Tunapousoma, basi nawe fuatiliza kusoma kwake.
19Kisha ni juu yetu kuubainisha.
20Hasha! Bali nyinyi mnapenda maisha ya duniani.
21Na mnaacha maisha ya Akhera.
22Zipo nyuso siku hiyo zitakazong'ara.
23Zinamwangallia Mola wao Mlezi.
24Na zipo nyuso siku hiyo zitakazokunjana.
25Zitajua ya kuwa zitafikiwa na livunjalo uti wa mgongo.
26La, hasha! (Roho) itakapofikia kwenye mafupa ya koo.
27Na pakasemwa: Nani wa kumtibu (apone)?
28Na mwenyewe akajua kwa hakika kuwa huko ndiko kufariki.
29Na utakapoambatishwa muundi kwa muundi.
30Siku hiyo ndiyo kuchungwa kupelekwa kwa Mola wako Mlezi!
31Kwa sababu hakusadiki, wala hakusali.
32Bali alikanusha, na akageuka.
33Kisha akenda kwa ahali zake kwa matao.
34Ole wako, ole wako!
35Kisha ole wako, ole wako!
36Ati anadhani binadamu kuwa ataachwa bure?
37Kwani hakuwa yeye tone la manii lililoshushwa?
38Kisha akawa kidonge cha damu, tena Mwenyezi Mungu akamuumba na akamtengeneza vilivyo.
39Kisha akamfanya namna mbili, mwanamume na mwanamke.
40Je, huyo hakuwa ni Muweza wa kufufua wafu?