الحجرات
The Rooms • 18 ayahs • Medinan
بِسْمِ ٱللَّهِ ٱلرَّحْمَٰنِ ٱلرَّحِيمِ
1Enyi mlioamini! Msitangulie mbele ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia mno, Mwenye kujua zaidi.
2Enyi mlioamini! Msinyanyue sauti zenu kuliko sauti ya Nabii, wala msiseme naye kwa kelele kama mnavyosemezana nyinyi kwa nyinyi, visije vitendo vyenu vikaharibika, na hali hamtambui.
3Kwa hakika wale wanaoteremsha sauti zao mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, hao ndio Mwenyezi Mungu amezisafisha nyoyo zao kwa ucha Mungu. Hao watakuwa na maghfira na ujira mkubwa.
4Hakika hao wanaokuita nawe uko nyuma ya vyumba, wengi wao hawatumii akili.
5Na lau wao wangelingojea mpaka uwatokee, ingelikuwa heri kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghfira, Mwingi wa kurehemu.
6Enyi mlioamini! Akikujieni mpotovu na habari yoyote, ichunguzeni, msije mkawasibu watu kwa kutojua, na mkawa tena wenye kujuta kwa mliyoyatenda.
7Na jueni kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu yuko nanyi. Lau angeliwatii katika mambo mengi, bila ya shaka mngelitaabika. Lakini Mwenyezi Mungu amewapendezea Imani, na akaipamba katika nyoyo zenu, na amewafanya muuchukie ukafiri, na upotovu, na uasi. Hao ndio walioongoka.
8Kwa fadhila za Mwenyezi Mungu na neema zake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua mno, Mwenye hekima.
9Na ikiwa makundi mawili katika Waumini yanapigana, basi yapatanisheni. Na likiwa moja la hao linamdhulumu mwenziwe, basi lipigeni linalodhulumu mpaka lirejee kwenye amri ya Mwenyezi Mungu. Na likirudi, basi yapatanisheni kwa uadilifu. Na hukumuni kwa haki. Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wanaohukumu kwa haki.
10Hakika Waumini ni ndugu, basi patanisheni baina ya ndugu zenu, na mcheni Mwenyezi Mungu ili mrehemewe.
11Enyi mlioamini! Wanaume wasiwadharau wanaume wenzao, wala wanawake wasiwadharau wanawake wenzao. Huenda hao wakawa bora kuliko wao. Wala msivunjiane heshima, wala msiitane kwa majina ya kejeli. Ni uovu kutumia jina baya baada ya kwisha amini. Na wasiotubu, hao ndio wenye kudhulumu.
12Enyi mlioamini! Jiepusheni na dhana nyingi, kwani baadhi ya dhana ni dhambi. Wala msipelelezane, wala msisengenyane nyinyi kwa nyinyi. Je, yupo katika nyinyi anayependa kuila nyama ya nduguye aliyekufa? Mnalichukia hilo! Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kupokea toba mno, Mwingi wa kurehemu.
13Enyi watu! Hakika Sisi tumewaumba kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mcha Mungu zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua mno, Mwenye habari.
14Mabedui walisema: 'Tumeamini.' Sema: 'Hamjaamini, lakini semeni: 'Tumesilimu.' Kwani Imani haijaingia katika nyoyo zenu. Na mkimtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hatakupunguzieni chochote katika vitendo vyenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe mno, Mwingi wa kurehemu.'
15Hakika Waumini ni wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake tena wasitie shaka kabisa, na wakapigana Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali zao na nafsi zao. Hao ndio wakweli.
16Sema: 'Ati ndio mnamfundisha Mwenyezi Mungu Dini yenu, na hali Mwenyezi Mungu anayajua ya katika mbingu na ardhi, na Mwenyezi Mungu anajua vyema kila kitu?'
17Wanakusimbulia kuwa wamesilimu! Sema: 'Msinisimbulie kwa kusilimu kwenu. Bali Mwenyezi Mungu ndiye aliyewafanyia hisani kwa kukuongoeni kwenye Imani, ikiwa nyinyi ni wakweli.'
18Hakika Mwenyezi Mungu anajua siri za mbingu na ardhi. Na Mwenyezi Mungu anayaona mno myatendayo.