ق
Qaf • 45 ayahs • Meccan
بِسْمِ ٱللَّهِ ٱلرَّحْمَٰنِ ٱلرَّحِيمِ
1Qaaf.[1] Ninaapa kwa Qur-ani tukufu!
2Bali wanastaajabu kwamba amewafikia mwonyaji kutoka miongoni mwao, na wakasema makafiri: 'Hili ni jambo la ajabu!
3Ati tukifa na tukawa udongo...? Kurejea huko kuko mbali!'
4Hakika Sisi tunajua kiasi cha kila kinachopunguzwa na ardhi kutokana nao. Na kwetu kipo Kitabu kinachohifadhi vyema yote.
5Lakini waliikanusha Haki ilipowajia; kwa hivyo wamo katika mambo ya mchanganyiko.
6Je, hawaangalii mbingu zilizo juu yao! Vipi tulivyozijenga, na tukazipamba. Wala hazina nyufa.
7Na ardhi tumeitandaza na tukaiwekea milima, na tukaiotesha mimea mizuri ya kila namna.
8Yawe haya ni kifumbua macho na ukumbusho kwa kila mja mwenye kurejea (kwa Mwenyezi Mungu).
9Na tumeteremsha kutoka mbinguni maji yaliyobarikiwa, na kwa hayo tukaotesha mabustani na nafaka za kuvunwa.
10Na mitende mirefu yenye makole yaliyozaa kwa wingi.
11Ili iwe ni riziki kwa waja wangu. Na tukaifufua kwa maji nchi iliyokuwa imekufa. Kama hivyo ndivyo utakavyokuwa ufufuaji.
12Kabla yao walikadhibisha kaumu ya Nuhu na wakazi wa Rassi na Thamudi.
13Na A'di na Firauni na kaumu ya Luti.
14Na wakazi wa Machakani, na watu wa Tubbaa'. Wote hao waliwakanusha Mitume, kwa hivyo onyo likathibitika juu yao.
15Kwani tulichoka kwa kuumba mara ya kwanza? Bali wao wamo katika shaka tu juu ya umbo jipya.
16Na hakika tulimuumba mtu, nasi tunayajua yanayomtia wasiwasi katika nafsi yake. Na Sisi tuko karibu naye kuliko mshipa wa shingoni mwake.
17Wanapopokea wapokeaji wawili, wanaokaa kuliani na kushotoni.
18Hatamki neno ila karibu yake yupo mwangalizi tayari.
19Na uchungu wa kutoka roho utamjia kwa haki. Hayo ndiyo uliyokuwa ukiyakimbia.
20Na litapulizwa baragumu. Hiyo ndiyo Siku ya Miadi.
21Na kila nafsi itakuja na pamoja nayo mchungaji na shahidi.
22(Aambiwe): 'Kwa hakika ulikuwa umeghafilika mbali na haya. Basi leo tumekuondolea pazia lako, na kwa hivyo kuona kwako leo ni kukali mno.'
23Na mwenzake atasema: 'Huyu niliye naye mimi keshatayarishwa.
24Mtupeni katika Jahanamu kila kafiri mkubwa mkaidi.
25Akatazaye mno heri, arukaye mipaka, mwenye kutia shaka.
26Aliyeweka mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu. Basi mtupeni katika adhabu kali.'
27Mwenzake aseme: 'Ewe Mola wetu Mlezi! Sikumpoteza mimi, bali yeye mwenyewe alikuwa katika upotovu wa mbali.'
28(Mwenyezi Mungu) aseme: 'Msigombane mbele yangu. Tayari niliwaletea mbele onyo langu.
29Mbele yangu haibadilishwi kauli, wala Mimi siwadhulumu waja wangu.
30Siku tutakapoiambia Jahanamu: 'Je, umejaa?' Nayo itasema: 'Je, kuna ziada?'
31Na Bustani ya mbinguni italetwa karibu mno kwa ajili ya wacha Mungu, haitakuwa mbali.
32Haya ndiyo mnayoahidiwa kwa kila mwenye kurejea mno kwa Mwenyezi Mungu na akajilinda vyema.
33Mwenye kumwogopa mno Mwingi wa rehema hali kuwa hamwoni, na akaja kwa moyo uliotubia.
34(Ataambiwa) ingieni humo kwa salama. Hiyo ndiyo siku ya kudumu daima dawamu.
35Humo watapata wakitakacho, na kwetu yako ya ziada.
36Na kaumu ngapi tuliziangamiza kabla yao, waliokuwa na nguvu zaidi kuliko hawa! Nao walitanga tanga katika nchi nyingi. Je, walipata pa kukimbilia?
37Hakika katika hayo upo ukumbusho kwa mwenye moyo au akatega sikio naye yupo anashuhudia.
38Na bila ya shaka Sisi tumeziumba mbingu na ardhi na vilivyo baina yake katika siku sita; na wala hayakutugusa machovu yoyote.[1]
39Basi vumilia kwa hayo wasemayo, na mtakase kwa kumsifu Mola wako Mlezi kabla ya kuchomoza jua na kabla ya kuchwa.
40Na katika usiku pia mtakase, na baada ya kusujudu.
41Na sikiliza siku atakaponadi mwenye kunadi kutoka mahali karibu.
42Siku watakaposikia ukelele wa haki. Hiyo ndiyo siku ya kufufuka.
43Hakika Sisi tunahuisha na tunafisha, na kwetu Sisi ndio marejeo.
44Siku itapowapasukia ardhi mbio mbio! Mkusanyo huo kwetu ni mwepesi.
45Sisi tunajua kabisa wayasemayo. Wala wewe si mwenye kuwatawalia kwa ujabari. Basi mkumbushe kwa Qur-ani anayeliogopa onyo.