القمر
The Moon • 55 ayahs • Meccan
بِسْمِ ٱللَّهِ ٱلرَّحْمَٰنِ ٱلرَّحِيمِ
1Saa imekaribia, na mwezi umepasuka!
2Na wakiona Ishara, hugeuka upande na husema: 'Huu uchawi tu unazidi kuendelea.'
3Na wamekanusha na wamefuata matamanio yao. Na kila jambo ni lenye kuthibiti.
4Na bila ya shaka zimewajia habari zenye makaripio.
5Hekima kamili; lakini maonyo hayafai kitu!
6Basi jiepushe nao. Siku atakapoita mwitaji kuliendea jambo linalochusha.
7Macho yao yatainama; watatoka makaburini kama nzige waliotawanyika.
8Wanamkimbilia mwitaji, na makafiri wanasema: 'Hii ni siku ngumu.'
9Kabla yao kaumu ya Nuhu walikanusha; wakamkanusha mja wetu, na wakasema ni mwendawazimu, na akakaripiwa.
10Basi akamwomba Mola wake Mlezi akasema: 'Kwa hakika mimi nimeshindwa, basi ninusuru!'
11Basi tukaifungua milango ya mbingu kwa maji yanayomiminika.
12Na tukazipasua ardhi kwa chemichemi, yakakutana maji kwa jambo lililokwisha pangwa.
13Na tukambeba kwenye safina ya mbao na kamba.
14Ikawa inakwenda kwa macho yetu, kuwa ni malipo kwa aliyekuwa amekanushwa.
15Na bila ya shaka tuliiacha iwe ni Ishara. Lakini je, yupo anayekumbuka?
16Basi ilikuwaje adhabu yangu, na maonyo yangu.
17Na bila ya shaka Sisi tumeifanya Qur-ani iwe nyepesi kufahamika. Lakini yupo anayekumbuka?
18Kina 'Adi walikanusha. Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu?
19Hakika Sisi tuliwatumia upepo wa kimbunga katika siku korofi mfululizo.
20Ukiwang'oa watu kama vigogo vya mitende vilivyong'olewa.
21Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu?
22Na bila ya shaka Sisi tumeifanya Qur-ani nyepesi kufahamika; lakini yupo anayekumbuka?
23Thamudi waliwakanusha Waonyaji.
24Wakasema: 'Ati tumfuate binadamu mmoja katika sisi? Basi hivyo sisi tutakuwa katika upotovu na kichaa!
25Ni yeye tu aliyeteremshiwa huo ukumbusho kati yetu sote? Bali huyu ni mwongo mno, mshari mkubwa!
26Kesho watajua ni nani huyo mwongo mno, mshari mkubwa.
27Hakika Sisi tutawatumia ngamia jike ili kuwajaribu, basi watazame vyema tu na ustahamili.
28Na waambie kwamba hakika maji yatagawanywa baina yao; kila sehemu ya maji itahudhuriwa na aliyehusika.
29Basi wakamwita mtu wao akaja akamchinja.
30Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu!
31Hakika Sisi tuliwatumia ukelele mmoja tu, wakawa kama mabuwa ya kujengea ua.
32Na bila ya shaka Sisi tumeifanya Qur-ani iwe nyepesi kwa kukumbuka, lakini yupo akumbukaye?
33Kaumu Lut'i nao waliwakadhibisha Waonyaji.
34Hakika Sisi tukawatumia kimbunga cha vijiwe, isipokuwa wafuasi wa Lut'i. Hao tuliwaokoa karibu na alfajiri.
35Kwa neema inayotoka kwetu. Hivyo ndivyo tumlipavyo anayeshukuru.
36Na hakika yeye aliwaonya adhabu yetu; lakini wao waliyatilia shaka hayo maonyo.
37Na walimtaka awape wageni wake. Tukayapofua macho yao, na tukawaambia: 'Onjeni basi adhabu na maonyo yangu!'
38Na iliwafikia wakati wa asubuhi adhabu yangu ya kuendelea.
39Basi onjeni adhabu na maonyo yangu!
40Na hakika tumeisahilisha Qur-ani kuikumbuka. Lakini yupo anayekumbuka?
41Na Waonyaji waliwajia watu wa Firauni.
42Walizikadhibisha Ishara zetu zote, nasi tukawashika mshiko wa Mwenye nguvu, Mwenye uwezo.
43Je, makafiri wenu ni bora kuliko hao, au yameandikwa vitabuni kuwa nyinyi hamtiwi makosani?
44Au ndiyo wanasema: 'Sisi ni wengi tutashinda tu.'
45Wingi wao huu utashindwa, na wao watasukumwa nyuma.
46Bali Saa ya Kiyama ndiyo miadi yao, na Saa hiyo ni nzito zaidi na chungu zaidi.
47Hakika wakosefu wamo katika upotovu na wazimu.
48Siku watakapokokotwa Motoni kifudifudi waambiwe: 'Onjeni mguso wa Saqar!'
49Kwa hakika Sisi tumekiumba kila kitu kwa kipimo.
50Na amri yetu haikuwa ila ni moja tu, kama kupepesa jicho.
51Na bila ya shaka tumekwisha waangamiza wenzenu. Lakini yupo anayekumbuka?
52Na kila jambo walilolifanya limo vitabuni.
53Na kila kidogo na kikubwa kimeandikwa.
54Hakika wacha Mungu watakuwa katika Mabustani na mito.
55Katika mahali pa kukalia pa haki kwa Mfalme Mwenye uweza.