الطور
The Mount • 49 ayahs • Meccan
بِسْمِ ٱللَّهِ ٱلرَّحْمَٰنِ ٱلرَّحِيمِ
1Ninaapa kwa mlima wa T'ur.
2Na Kitabu kilichoandikwa.
3Katika ngozi iliyokunjuliwa.
4Na kwa Nyumba iliyojengwa.
5Na kwa dari iliyonyanyuliwa.
6Na kwa bahari iliyojazwa.
7Hakika adhabu ya Mola wako Mlezi hapana shaka itatokea.
8Hapana wa kuizuia.
9Siku zitakapotikisika mbingu kwa mtikiso.
10Na milima iwe inakwenda kwa mwendo mkubwa.
11Basi ole wao siku hiyo hao wanaokadhibisha.
12Ambao wanacheza katika mambo ya upuuzi.
13Siku watakaposukumwa kwenye Moto kwa msukumo wa nguvu.
14(Waambiwe): Huu ndio ule Moto mliokuwa mkiukadhibisha!
15Je, huu ni uchawi, au hamwoni tu?
16Uingieni, mkistahamili au msistahamili - ni mamoja kwenu. Hakika mnalipwa kwa mliyokuwa mkiyatenda.
17Hakika wacha Mungu watakuwa katika Mabustani na neema.
18Wakifurahi kwa yale aliyowapa Mola wao Mlezi. Na Mola wao Mlezi atawalinda kutokana na adhabu ya Motoni.
19Kuleni na kunyweni kwa raha kabisa kwa sababu ya mliyokuwa mkiyatenda.
20Watakuwa wameegemea juu ya viti vya enzi vilivyopangwa kwa safu. Na tutawaoza mahurulaini.
21Na wale walioamini na dhuriya zao wakawafuata kwa Imani, tutawakutanisha nao dhuriya zao, na wala hatutawapunja hata kidogo katika vitendo vyao. Kila mtu lazima atapata alichokichuma.
22Na tutawapa matunda, na nyama kama watakavyopenda.
23Watapeana humo bilauri zisizo na vinywaji vya kuleta maneno ya upuuzi wala dhambi.
24Iwe wanawapitia watumishi wao kama kwamba ni lulu zilizomo katika chaza.
25Wataelekeana wakiulizana.
26Waseme: Hakika tulikuwa zamani pamoja na ahali zetu tukiogopa mno.
27Basi Mwenyezi Mungu akatufanyia hisani na akatulinda mbali adhabu ya upepo wa Moto.
28Hakika sisi zamani tulikuwa tukimwomba Yeye tu. Hakika Yeye ndiye Mwema Mwingi wa kurehemu.
29Basi kumbusha! Kwani wewe, kwa neema ya Mola wako Mlezi, si kuhani wala mwendawazimu.
30Au wanasema: Huyu ni mtunga mashairi, tunamtarajia kupatilizwa na dahari.
31Sema: Tarajieni, na mimi pia ni pamoja nanyi katika kutarajia.
32Au hizo akili zao ndio zinawaamrisha haya, au wao basi ni watu majeuri tu?
33Au ndiyo wanasema: 'Ameitunga hii!' Bali basi tu hawaamini!
34Basi nawalete masimulizi kama haya ikiwa wao wanasema kweli.
35Au wao wameumbwa pasipo kutokana na kitu chochote, au ni wao ndio waumbaji?
36Au wao wameziumba mbingu na ardhi? Bali hawana yakini.
37Au wanazo hazina za Mola wako Mlezi au wao ndio wenye madaraka?
38Au wanazo ngazi za kusikilizia? Basi huyo msikilizaji wao na alete hoja iliyo wazi!
39Au Yeye Mwenyezi Mungu ana wasichana, na nyinyi ndio mna wavulana?
40Au wewe unawaomba ujira, na kwa hivyo ndio wanaelemewa na uzito wa gharama?
41Au wanayo elimu ya ghaibu, nao wameandika?
42Au wanataka kufanya vitimbi tu? Lakini hao waliokufuru ndio watakaotegeka.
43Au wanaye mungu asiyekuwa Mwenyezi Mungu? Ametakasika Mwenyezi Mungu mbali na hao wanaowashirikisha naye.
44Na hata wangeona pande linatoka mbinguni linaanguka wangesema: Ni mawingu yaliyobebana.
45Basi waache mpaka wakutane na siku yao watakapohilikishwa.
46Siku ambayo hila zao hazitawafaa hata kidogo, wala wao hawatanusuriwa.
47Na hakika wale waliodhulumu watapata adhabu nyingine isiyokuwa hii, lakini wengi wao hawajui.
48Na ingojee hukumu ya Mola wako Mlezi. Kwani wewe hakika uko mbele ya macho yetu.
49Na usiku pia mtakase, na zinapokuchwa nyota.