الزمر
The Groups • 75 ayahs • Meccan
بِسْمِ ٱللَّهِ ٱلرَّحْمَٰنِ ٱلرَّحِيمِ
1Uteremsho wa Kitabu hiki umetokana na Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
2Hakika Sisi tumekuteremshia Kitabu hiki kwa Haki. Basi muabudu Mwenyezi Mungu ukimsafia Dini Yeye tu.
3Hakika Dini Safi ni ya Mwenyezi Mungu tu. Na wale wanaowafanya wenginewe kuwa ni walinzi wakisema: Sisi hatuwaabudu ila wapate kutujongeza tu kumkaribia Mwenyezi Mungu - Hakika Mwenyezi Mungu atahukumu baina yao katika wanayohitalifiana. Hakika Mwenyezi Mungu hamwongoi aliye mwongo kafiri.
4Lau kuwa Mwenyezi Mungu angelitaka kuwa na mwana, basi bila ya shaka angeliteua amtakaye katika aliowaumba. Ametakasika na hayo! Yeye ni Mwenyezi Mungu Mmoja, Mtenda atakalo.
5Ameumba mbingu na ardhi kwa Haki. Hufunika usiku juu ya mchana, na hufunika mchana juu ya usiku. Na amefanya jua na mwezi vitumike. Kila kimojapo kinakwenda kwa kipindi kilichowekewa. Jueni mtanabahi! Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kusamehe!
6Amewaumba kutokana na nafsi moja. Kisha akamfanya mwenziwe katika nafsi ile ile. Na akawaletea wanyama wa mifugo jozi nane. Anawaumba katika matumbo ya mama zenu, umbo baada ya umbo, katika viza vitatu. Huyu ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu Mlezi. Ufalme ni wake. Hapana mungu isipokuwa Yeye. Basi nyinyi mnageuzwa wapi?
7Mkikufuru basi Mwenyezi Mungu si mwenye haja nanyi, lakini hafurahii kufuru kwa waja wake. Na mkishukuru Yeye hufurahika nanyi. Wala mbebaji habebi mzigo wa mwingine. Kisha marejeo yenu ni kwa Mola wenu Mlezi. Hapo atawaambia mliyokuwa mkiyafanya. Hakika Yeye ni Mwenye kuyajua vyema yaliyomo vifuani.
8Na taabu inapomfikia mtu humwomba Mola wake Mlezi naye ameelekea kwake. Kisha akimpa neema kutoka kwake, husahau yale aliyokuwa akimwomba zamani, na akamfanyia Mwenyezi Mungu washirika ili apoteze watu mbali na njia yake. Sema: Starehe na ukafiri wako kwa muda mchache. Kwani hakika wewe utakuwa miongoni mwa watu wa Motoni.
9Je, afanyaye ibada nyakati za usiku kwa kusujudu na kusimama akitahadhari na Akhera, na akitaraji rehema za Mola wake Mlezi... Sema: Ati watakuwa sawa wale wanaojua na wale wasiojua? Hakika wanaokumbuka ni watu wenye akili.
10Sema: Enyi waja wangu mlioamini! Mcheni Mola wenu Mlezi. Wale wafanyao wema katika dunia hii watapata wema. Na ardhi ya Mwenyezi Mungu ni kunjufu. Hakika wenye subira watapewa ujira wao bila ya hisabu.
11Sema: Hakika mimi nimeamrishwa nimuabudu Mwenyezi Mungu kwa kumsafishia Dini Yeye tu.
12Na nimeamrishwa niwe wa mwanzo wa Waislamu.
13Sema: Hakika mimi ninaogopa adhabu ya Siku Kubwa nikimuasi Mola wangu Mlezi.
14Sema: Mwenyezi Mungu tu namuabudu kwa kumsafishia Yeye tu Dini yangu.
15Basi nyinyi abuduni mpendacho badala yake Yeye. Sema: Hakika waliohasirika ni wale waliojihasiri na ahali zao Siku ya Kiyama. Tambueni kuwa hiyo ndiyo hasara iliyo dhahiri.
16Yatawekwa juu yao matabaka ya moto, na chini yao matabaka. Kwa hayo Mwenyezi Mungu anawahofisha waja wake. Enyi waja wangu! Nicheni Mimi!
17Na wale wanaojiepusha ibada potovu, na wakarejea kwa Mwenyezi Mungu, watapata bishara njema. Basi wabashirie waja wangu.
18Ambao husikiliza maneno, wakafuata lililo bora yake. Hao ndio aliowaongoa Mwenyezi Mungu, na hao ndio wenye akili.
19Je, yule mwenye kustahiki hukumu ya adhabu, je, wewe unaweza kumwokoa aliye katika Moto?
20Lakini waliomcha Mola wao Mlezi watapata ghorofa zilizojengwa juu ya ghorofa; chini yake hupita mito. Ndiyo ahadi ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu havunji ahadi yake.
21Je, huoni kwamba Mwenyezi Mungu ameteremsha maji kutoka mbinguni. Kisha akayapitisha kwenye chemchemi katika ardhi, kisha kwa maji hayo akatoa mimea yenye rangi mbalimbali? Kisha hunyauka ukaiona imekuwa kimanjano, na kisha huifanya mapepe. Bila ya shaka katika hayo upo ukumbusho kwa wenye akili.
22Je, yule ambaye Mwenyezi Mungu amemfungulia kifua chake kwa Uislamu, na akawa yuko kwenye nuru itokayo kwa Mola wake Mlezi (ni sawa na mwenye moyo mgumu?) Basi ole wao wenye nyoyo ngumu zisizomkumbuka Mwenyezi Mungu! Hao wamo katika upotovu wa dhahiri.
23Mwenyezi Mungu ameteremsha hadithi nzuri kabisa, Kitabu chenye kufanana na kukaririwa; husisimua kwacho ngozi za wenye kumhofu Mola wao Mlezi. Kisha ngozi zao na nyoyo zao hulainika kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Huo ndio uongofu wa Mwenyezi Mungu, na kwa huo humwongoa amtakaye. Na ambaye ameachwa na Mwenyezi Mungu kupotea, basi hapana wa kumwongoa.
24Je, atakayekuwa anapambana kwa uso wake na adhabu mbaya kabisa Siku ya Kiyama, (ni sawa na watenda wema?) Na wataambiwa wenye kudhulumu: Onjeni hayo mliyokuwa mkiyachuma!
25Waliokuwa kabla yao walikadhibisha, na ikawajia adhabu kutoka pahala wasipopatambua.
26Basi Mwenyezi Mungu akawaonjesha hizaya katika uhai wa duniani. Na bila ya shaka adhabu ya Akhera ni kubwa zaidi; laiti wangelijua!
27Na bila ya shaka tumewapigia watu mifano ya kila namna katika hii Qur-ani ili wapate kukumbuka.
28Qur-ani ya Kiarabu isiyo na upogo, ili wamche Mungu.
29Mwenyezi Mungu amepiga mfano wa mtu mwenye mabwana washirika wanaogombana, na wa mtu mwingine aliyehusika na bwana mmoja tu. Je, wako sawa katika hali zao? Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu! Lakini wengi wao hawajui.
30Kwa hakika wewe utakufa, na wao watakufa.
31Kisha bila ya shaka mtagombana Siku ya Kiyama mbele ya Mola wenu Mlezi.
32Basi ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule aliyemsingizia uongo Mwenyezi Mungu na akaukadhibisha ukweli ulipomfikia? Je, siyo katika Jahannamu makazi ya hao makafiri?
33Na aliyeuleta ukweli na akausadiki - hao ndio wacha Mungu.
34Watapata watakachotaka kwa Mola wao Mlezi. Hayo ndiyo malipo ya watendao mema.
35Ili Mwenyezi Mungu awafutie ukomo wa uovu walioufanya na awalipe ujira wao kwa mujibu wa ukomo wa wema waliokuwa wakiutenda.
36Je, Mwenyezi Mungu si wa kumtosheleza mja wake? Na ati wanakutishia kwa hao wenginewe wasiokuwa Yeye! Na aliyepotezwa na Mwenyezi Mungu, basi hana wa kumwongoa.
37Na ambaye Mwenyezi Mungu anamwongoa, basi hana wa kumpotoa. Je, Mwenyezi Mungu si Mwenye nguvu, anayeweza kulipiza?
38Na ukiwauliza: Ni nani aliyeziumba mbingu na ardhi. Bila ya shaka watasema: Mwenyezi Mungu. Sema: Je, mnawaonaje wale mnaowaomba badala ya Mwenyezi Mungu, ikiwa Mwenyezi Mungu akitaka kunidhuru, wao wanaweza kuniondolea dhara yake? Au akitaka kunirehemu, je, wao wanaweza kuzuia rehema yake? Sema: Mwenyezi Mungu ananitosheleza. Kwake Yeye na wategemee wanaotegemea.
39Sema: Enyi watu wangu! Fanyeni muwezavyo, mimi pia nafanya. Basi mtakuja ona.
40Ni nani itakayemfikia adhabu ya kumhizi na itakayemshukia adhabu ya daima.
41Hakika Sisi tumekuteremshia Kitabu kwa ajili ya watu wote kwa Haki. Kwa hivyo, mwenye kuongoka, ni kwa faida ya nafsi yake. Na mwenye kupotoka, bila ya shaka amepotoka kwa hasara yake. Na wewe si mlinzi juu yao.
42Mwenyezi Mungu huzipokea roho zinapokufa. Na zile zisizokufa wakati wa kulala kwake, huzishika zilizohukumiwa kufa, na huzirudisha nyingine mpaka ufike wakati uliowekwa. Hakika katika hayo bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanaofikiri.
43Au ndio wanachukua waombezi badala ya Mwenyezi Mungu? Sema: Ingawa hawana mamlaka juu ya kitu chochote, wala hawatambui lolote.
44Sema: Uombezi wote uko kwa Mwenyezi Mungu. Ni wake Yeye tu ufalme wa mbingu na ardhi. Kisha mtarejeshwa kwake.
45Na anapotajwa Mwenyezi Mungu peke yake, nyoyo za wasioiamini Akhera huchafuka. Na wanapotajwa wenginewe wasiokuwa Yeye, basi wao hufurahi mno.
46Sema: Ewe Mwenyezi Mungu! Muumba mbingu na ardhi! Mjuzi wa yasiyoonekana na yanayoonekana! Wewe utahukumu baina ya waja wako katika yale waliyokuwa wakihitalifiana.
47Na lau kuwa wale waliodhulumu wangelikuwa na vyote vilivyomo duniani na pamoja navyo vingine kama hivyo, bila ya shaka wangelivitoa kujikomboa kutokana na adhabu mbaya hiyo Siku ya Kiyama. Na yatawadhihirikia kwa Mwenyezi Mungu wasiyokuwa wakiyatarajia.
48Na utawadhihirikia ubaya wa yale waliyoyachuma, na yatawazingira na kuwafika yale waliyokuwa wakiyafanyia mzaha.
49Na dhara inapomgusa mtu, hutuomba. Kisha tunapompa neema zitokazo kwetu, husema: Nimepewa haya kwa sababu ya elimu yangu. Sivyo! Huo ni mtihani! Lakini wengi wao hawajui!
50Waliyasema haya wale waliokuwa kabla yao, lakini hayakuwafaa waliyokuwa wakiyachuma.
51Basi ukawasibu uovu wa yale waliyoyachuma. Na wale waliodhulumu miongoni mwa hawa utawasibu uovu wa yale waliyoyachuma vile vile. Nao si wenye kushinda.
52Kwani wao hawajui kwamba Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye na kumkunjia? Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanaoamini.
53Sema: Enyi waja wangu waliojidhulumu nafsi zao! Msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote. Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
54Na rejeeni kwa Mola wenu Mlezi, na silimuni kwake, kabla ya kuwajieni adhabu. Kisha hapo hamtanusuriwa.
55Na fuateni yaliyo bora kabisa katika yale yaliyoteremshwa kwenu kutoka kwa Mola wenu Mlezi, kabla haijakujieni adhabu kwa ghafla, na hali hamtambui.
56Isije ikasema nafsi: Ee majuto yangu kwa yale niliyopoteza upande wa Mwenyezi Mungu, na hakika nilikuwa miongoni mwa wanaofanya maskhara!
57Au ikasema: Ingelikuwa Mwenyezi Mungu ameniongoa, bila ya shaka ningelikuwa miongoni mwa wenye kumcha Mungu.
58Au ikasema inapoona adhabu: Lau kuwa ningelipata fursa nyingine, ningelikuwa miongoni mwa wafanya mema.
59Wapi! Bila ya shaka zilikujia Ishara zangu, nawe ukazikadhibisha, na ukajivuna, na ukawa miongoni mwa makafiri!
60Na Siku ya Kiyama utawaona waliomsingizia uongo Mwenyezi Mungu nyuso zao zimesawijika. Je, si katika Jahannamu makazi ya wanaotakabari?
61Na Mwenyezi Mungu atawaokoa wenye kujikinga kwa ajili ya kufuzu kwao. Hapana uovu utakaowagusa, wala hawatahuzunika.
62Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wa kila kitu, na Yeye ndiye Mlinzi juu ya kila kitu.
63Yeye anazo funguo za mbingu na ardhi. Na wale waliozikataa Ishara za Mwenyezi Mungu, hao ndio wenye kuhasiri.
64Sema: Je, mnaniamrisha nimuabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu, enyi majahili?
65Na kwa yakini yamefunuliwa kwako na kwa waliokuwa kabla yako: Bila ya shaka ukimshirikisha Mwenyezi Mungu matendo yako yataharibika, na lazima utakuwa miongoni mwa wenye kuhasiri.
66Bali muabudu Mwenyezi Mungu tu, na uwe miongoni mwa wenye kushukuru.
67Na wala hawakumheshimu Mwenyezi Mungu kama anavyostahiki kuheshimiwa. Na Siku ya Kiyama ardhi yote itakuwa mkononi mwake, na mbingu zitakunjwa katika mkono wake wa kiume. Ametakasika na Ametukuka na hayo wanayomshirikisha nayo.
68Na litapulizwa barugumu, wazimie waliomo mbinguni na waliomo katika ardhi, isipokuwa aliyemtaka Mwenyezi Mungu. Kisha litapulizwa mara nyingine. Hapo watainuka wawe wanangojea.
69Na ardhi itang'ara kwa Nuru ya Mola wake Mlezi, na Kitabu kitawekwa, na wataletwa Manabii na mashahidi, na patahukumiwa baina yao kwa haki, wala hawatadhulumiwa.
70Na kila nafsi italipwa kwa yale iliyoyafanya, na Yeye anayajua sana wanayoyatenda.
71Na wale waliokufuru wataongozwa kuendea Jahannamu kwa makundi. Mpaka watakapoifikia, itafunguliwa milango yake, na walinzi wake watawaambia: Kwani hawakukujilieni Mitume miongoni mwenu wakikusomeeni Aya za Mola wenu Mlezi na kukuonyeni mkutano wa siku yenu hii? Watasema: Kwani! Lakini limekwisha thibiti neno la adhabu juu ya makafiri.
72Itasemwa: Ingieni milango ya Jahannamu mdumu humo. Basi nayo ni ubaya ulioje wa makazi ya wanaotakabari!
73Na wale waliomcha Mola wao Mlezi wataongozwa kuendea Peponi kwa makundi, mpaka watakapofikia, nayo milango yake imekwisha funguliwa. Walinzi wake watawaambia: Amani iwe juu yenu! Mmetahirika. Basi ingieni humu mkae milele.
74Nao watasema: Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu aliyetutimizia ahadi yake, na akaturithisha ardhi, tunakaa katika Bustani popote tupendapo. Basi ni malipo mazuri yaliyoje ya watendao!
75Na utawaona Malaika wakizunguka pembeni mwa Kiti cha enzi cha Mwenyezi Mungu, wakimtakasa na kumsifu Mola wao Mlezi. Na patahukumiwa baina yao kwa haki na patasemwa: Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote!