الأنبياء
The Prophets • 112 ayahs • Meccan
بِسْمِ ٱللَّهِ ٱلرَّحْمَٰنِ ٱلرَّحِيمِ
1Imewakaribia watu hesabu yao, nao wako katika kughafilika wanapuuza.
2Hauwajii ukumbusho mpya kutoka kwa Mola wao Mlezi isipokuwa huusikiliza na huku wanafanya mchezo.
3Zimeghafilika nyoyo zao. Na wale waliodhulumu hunong'onezana kwa siri: Ni nani huyu isipokuwa ni mtu tu kama nyinyi! Je, mnauendea uchawi ilhali nyinyi mnaona?
4Alisema: Mola wangu Mlezi anayajua yasemwayo mbinguni na katika ardhi. Na Yeye ni Mwenye kusikia yote, Mwenye kujua vyema.
5Lakini wao walisema: "Hizo ni ndoto za ovyo ovyo, bali amezizua tu, bali huyo ni mtunga mashairi. Basi atuletee miujiza kama walivyotumwa wale wa mwanzo."
6Hawakuamini kabla yao watu wa mji wowote tuliouangamiza. Basi, je, hawa ndio wataamini?
7Na hatukuwatuma kabla yako isipokuwa wanaume tuliowafunulia ufunuo (wahyi). Basi waulizeni wenye elimu ikiwa nyinyi hamjui.
8Wala hatukuwafanya miili isiyokula chakula, wala hawakuwa wenye kuishi milele.
9Kisha tukawatimizia miadi, na tukawaokoa wao na wale tuliowataka, na tukawaangamiza wale waliopitiliza mipaka.
10Na hakika tumewateremshia Kitabu ambacho ndani yake kuna ukumbusho wenu. Je, hamtumii akili?
11Na ni mingapi katika miji iliyokuwa ikidhulumu tumeiteketeza, na tukawaanzisha baada yao kaumu wengine.
12Basi walipoihisi adhabu yetu, tazama, wakaanza kuikimbia.
13Msikimbie! Na rejeeni kwenye yale yale mliyostareheshwa kwayo, na maskani zenu, ili mpate kuulizwa!
14Wakasema: "Ole wetu! Hakika sisi tulikuwa madhalimu."
15Basi hakikuacha hicho kuwa ndicho kilio chao mpaka tukawafanya kama waliofyekwa, wamezimika.
16Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyo baina ya hivyo kwa mchezo.
17Kama tungelitaka kufanya pumbao, tungejifanyia Sisi wenyewe, lau kwamba tungelikuwa ni wafanyao hivyo.
18Bali tunaitupa haki juu ya batili, ikaivunja na mara ikatoweka. Na ole wenu kwa mnayoyazua.
19Na ni vyake Yeye tu vilivyomo mbinguni na katika ardhi. Na wale walioko kwake hawafanyi kiburi wakaacha kumuabudu, wala hawachoki.
20Wanamtakasa usiku na mchana, wala hawanyong'onyei.
21Au wamejifanyia miungu katika ardhi inayofufua?
22Lau wangelikuwamo humo miungu wengine isipokuwa Mwenyezi Mungu, basi bila ya shaka hizo mbingu na ardhi zingeliharibika. Subhanallah (Ametakasika Mwenyezi Mungu), Bwana wa Kiti cha Enzi mbali na hayo wanayoyazua.
23Yeye haulizwi kwa ayatendayo, na wao ndio wanaoulizwa kwa wayatendayo.
24Au wamejifanyia miungu mingine badala yake? Sema: Leteni ushahidi wenu! Haya ni ukumbusho wa hawa walio pamoja nami, na ukumbusho wa walio kabla yangu. Lakini wengi wao hawaijui haki, na kwa hivyo wanapeana mgongo.
25Na hatukumtuma kabla yako Mtume yeyote isipokuwa tulimfunulia ya kwamba hakuna mungu isipokuwa Mimi. Basi niabuduni Mimi tu.
26Na walisema: Arrahman (Mwingi wa rehema) alijifanyia mwana! Subhanahu (Ametakasika mbali na hayo!) Bali hao (wanaowaita wana) ni waja waliotukuzwa.
27Hawamtangulii kwa neno, nao wanafanya amri zake.
28Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao. Wala hawamfanyii yeyote uombezi isipokuwa yule anayemridhia Yeye, nao kwa sababu ya kumhofu wanaogopa mno.
29Na yeyote kati yao atakayesema: "Hakika mimi ni mungu, badala yake", basi huyo tutamlipa Jahannamu. Hivyo ndivyo tuwalipavyo madhalimu.
30Je, hao waliokufuru hawakuona kwamba mbingu na ardhi zilikuwa zimeambatana, kisha Sisi tukazibandua? Na tukafanya kwa maji kila kilicho hai? Basi je, hawaamini?
31Na tukaweka katika ardhi milima iliyo thabiti ili isiwayumbishe, na tukaweka humo njia pana ili wapate kuongoka.
32Na tukaifanya mbingu kuwa dari iliyohifadhiwa, lakini wanazipuuza Ishara zake.
33Na Yeye ndiye aliyeumba usiku na mchana na jua na mwezi, vyote katika anga vinaogelea.
34Nasi hatukumfanya mwanadamu yeyote kabla yako kuwa na uhai wa milele. Basi je, ukifa wewe, wao wataishi milele?
35Kila nafsi itaonja mauti; na tunawajaribu kwa mtihani wa maovu na heri. Na kwetu Sisi mtarejeshwa.
36Na wanapokuona wale waliokufuru, hawakufanyi wewe isipokuwa ni kitu cha masihara tu, (wakisema): Je, huyu ndiye anayeitaja miungu yenu? Na hali wao wanakufuru kumkumbuka Arrahman (Mwingi wa rehema)!
37Mwanadamu ameumbwa na haraka. Nitawaonyesha Ishara zangu. Basi msiniharakishe.
38Na wanasema: Ahadi hii itatokea lini, ikiwa nyinyi ni wakweli?
39Lau wangelijua wale waliokufuru wakati ambao hawatauzuia Moto kwenye nyuso zao wala migongo yao, na wala hawatanusuriwa!
40Bali itawafikia kwa ghafla, na itawashitua na wala hawataweza kuirudisha, wala hawatapewa muhula!
41Na Mitume walio kabla yako walikwishadhihakiwa. Kwa hivyo wale waliowafanyia masihara yaliwafika yale waliyokuwa wakiyafanyia dhihaka.
42Sema: Ni nani anayewalinda usiku na mchana mbali na Arrahmani (Mwingi wa rehema)? Bali wao wanapuuza kumkumbuka Mola wao Mlezi.
43Au wao wanao miungu watakaoweza kuwakinga kutokana nasi? Hao hawawezi kujinusuru wao wenyewe, wala hawatalindwa kutokana nasi!
44Bali tuliwastarehesha hawa na baba zao mpaka umri ukawa mrefu kwao. Je, hawaoni ya kwamba Sisi tunaijia ardhi tukiipunguza kutokea kwenye ncha zake? Basi je, hao ndio watashinda?
45Sema: Mimi ninawaonya kwa ufunuo (wahyi). Na viziwi hawasikii wito wanapoonywa.
46Na wanapoguswa na mpulizo mmoja tu wa adhabu itokayo kwa Mola wako Mlezi, bila ya shaka wao husema: Ole wetu! Hakika tulikuwa wenye kudhulumu.
47Nasi tutaweka mizani za uadilifu kwa Siku ya Kiyama. Basi nafsi haitadhulumiwa kitu chochote. Hata ikiwa ni uzito wa chembe ya khardali, tutaileta. Nasi tunatosha kuwa wenye kufanya hisabu sawasawa.
48Na kwa yakini tuliwapa Musa na Harun kipambanuzi, na mwangaza, na makumbusho kwa wacha Mungu,
49Ambao wanamhofu Mola wao Mlezi faraghani, na wanaiogopa Saa ya Kiyama.
50Na haya ni makumbusho yaliyobarikiwa, tuliyoyateremsha. Basi je! Mnayakataa?
51Na hakika tulikwishampa Ibrahim uongofu wake zamani, na tulikuwa tunamjua.
52Alipomwambia baba yake na watu wake: Ni nini haya masanamu mnayoshughulika kuyaabudu?
53Wakasema: Tuliwakuta baba zetu wakiyaabudu.
54Akasema: Bila ya shaka nyinyi na baba zenu mmekuwa katika upotovu ulio dhahiri.
55Wakasema: Je, umetujia kwa maneno ya kweli au wewe ni katika wachezao tu?
56Akasema: Bali Mola wenu Mlezi ni Mola Mlezi wa mbingu na ardhi ambaye ndiye aliyeziumba. Na mimi ni katika wenye kuyashuhudia hayo.
57Na ninaapa kwa Mwenyezi Mungu! Nitayafanyia vitimbi masanamu yenu haya baada ya mkishageuka kwenda zenu.
58Basi akayavunja vipande vipande, ila kubwa lao, ili wao walirudie.
59Wakasema: Ni nani aliyeifanyia haya miungu yetu? Hakika yeye ni katika waliodhulumu.
60Wakasema: Tumemsikia kijana mmoja akiwataja. Anaitwa Ibrahim.
61Wakasema: Mleteni mbele ya macho ya watu, ili wapate kumshuhudia!
62Wakasema: Je! Wewe umeifanyia haya miungu yetu, ewe Ibrahim?
63Akasema: Bali amefanya hayo huyu mkubwa wao. Basi waulizeni ikiwa wanaweza kutamka.
64Basi wakajirudia, wakasema: Hakika nyinyi mlikuwa madhalimu!
65Kisha wakarejea kwenye ule ule upotovu wao wakasema: Hakika wewe unajua kwamba hawa hawasemi.
66Akasema: Basi nyinyi mnawaabudu wasiokuwa Mwenyezi Mungu wasiowafaa kitu wala kuwadhuru?
67Aibu yenu nyinyi na hivyo mnavyoviabudu badala ya Mwenyezi Mungu! Basi nyinyi hamtii akilini?
68Wakasema: Mchomeni moto, na muinusuru miungu yenu, ikiwa nyinyi ni watendao jambo!
69Sisi tukasema: Ewe moto! Kuwa baridi na salama kwa Ibrahim!
70Wao walimkusudia maovu, lakini Sisi tukawafanya wao ndio waliohasiri zaidi.
71Na tukamwokoa yeye na Luuti, tukawapeleka kwenye nchi tuliyoibariki kwa ajili ya walimwengu wote.
72Naye tukampa Is-haq, na Yaaqub kuwa ni ziada. Na wote tukawafanya kuwa watu wema.
73Na tukawafanya maimamu wakiongoa watu kwa amri yetu. Na tukawafunulia watende heri, na washike Sala, na watoe Zaka; na walikuwa wanatuabudu Sisi tu.
74Na Lut tukampa hukumu na elimu na tukamwokoa kutokana na ule mji uliokuwa ukifanya machafu. Hakika hao walikuwa watu wabaya, wavukao mipaka.
75Na tukamuingiza katika rehema yetu. Hakika yeye ni miongoni mwa walio wema.
76Na Nuhu alipoita zamani, nasi tukamuitikia, na tukamwokoa yeye na watu wake kutokana na shida kubwa.
77Na tukamnusuru kutokana na watu waliozikanusha Ishara zetu. Hakika hao walikuwa watu wabaya. Basi tukawazamisha wote.
78Na Daud na Suleiman walipokata hukumu katika suala la konde walipolisha humo mbuzi wa watu usiku. Na Sisi tulikuwa wenye kushuhudia hukumu yao hiyo.
79Basi tukamfahamisha Suleiman. Na kila mmoja wao tulimpa hukumu na elimu. Na tuliifanya milima na ndege kuwa pamoja na Daud imnyenyekee na imtakase Mwenyezi Mungu. Na Sisi ndio tulioyafanya hayo.
80Na tukamfundisha kuunda mavazi ya vita kwa ajili yenu ili yawahifadhi katika kupigana kwenu. Je, mtakuwa wenye kushukuru?
81Na tukamsahilishia Suleiman upepo wa kimbunga uendao kwa amri yake kwenye ardhi tuliyoibariki. Na Sisi ndio tunaojua kila kitu.
82Na pia mashetani wanaompigia mbizi na kufanya kazi nyenginezo. Na Sisi tulikuwa walinzi wao.
83Na Ayyubu, alipomwita Mola wake Mlezi, akasema: Mimi yamenipata madhara. Na Wewe ndiye unayerehemu kuliko wote wanaorehemu.
84Basi tukamwitikia, na tukamwondolea madhara aliyokuwa nayo, na tukampa watu wake na mfano wao pamoja nao kuwa ni rehema inayotoka kwetu, na ukumbusho kwa wafanyao ibada.
85Na Ismail, na Idris, na Dhulkifli, wote walikuwa miongoni mwa wanaosubiri.
86Na tukawaingiza katika rehema yetu. Hakika wao walikuwa katika watu wema.
87Na Dhun-Nun alipoondoka hali ameghadhabika, na akadhani ya kwamba hatutamtia dhikini. Basi aliita katika giza: Hakuna mungu isipokuwa Wewe Subhanaka (Uliyetakasika). Hakika mimi nilikuwa miongoni mwa wenye kudhulumu.
88Basi tukamwitikia na tukamwokoa kutokana na dhiki. Na hivyo ndivyo tunavyowaokoa Waumini.
89Na Zakariya alipomwita Mola wake Mlezi: Mola wangu Mlezi! Usiniache peke yangu, na Wewe ndiye Mbora wa wanaorithi.
90Basi tukamwitikia, na tukampa Yahya na tukamponyeshea mkewe. Hakika wao walikuwa wepesi wa kutenda mema, na wakituomba kwa shauku na hofu. Nao walikuwa wakitunyenyekea.
91Na yule mwanamke aliyeulinda uke wake, na tukampulizia katika roho yetu, na tukamfanya yeye na mwanawe kuwa ni Ishara kwa walimwengu.
92Kwa hakika huu umma wenu ni umma mmoja, na Mimi ni Mola wenu Mlezi. Kwa hivyo niabuduni Mimi.
93Nao wakalikata jambo lao hili mapande mapande baina yao. Wote watarudi kwetu.
94Na atendaye mema naye ni Muumini, basi haitakataliwa juhudi yake. Na hakika Sisi tunamwandikia.
95Na haiwi kwa wana mji tuliouangamiza, ya kwamba hawatarejea.
96Mpaka watakapofunguliwa Yaajuju na Maajuju wakawa wanateremka haraka kutoka kwenye kila kilima.
97Na Miadi ya haki ikakaribia. Hapo ndipo yatakapokodoka macho ya waliokufuru (na watasema): Ole wetu! Bila ya shaka tulikuwa tumeghafilika mbali na haya, bali tulikuwa wenye kudhulumu.
98Hakika nyinyi na hao mnaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni kuni za Jahannamu; huko mtaingia tu.
99Lau kuwa hawa ni miungu, wasingelingia humo. Na wote watadumu humo.
100Lao wao humo ni kupiga mayowe, na wala hawatasikia (jinginelo).
101Ama wale ambao wema wetu umewatangulia, hao watatenganishwa na hayo.
102Hawatausikia mvumo wake, na wao watadumu katika yale ambayo nafsi zao zinayatamani.
103Hicho Kitisho Kikubwa hakitawahuzunisha. Na Malaika watawapokea (kwa kuwaambia): Hii ndiyo Siku yenu mliyokuwa mkiahidiwa!
104Siku tutakapozikunja mbingu kama mkunjo wa karatasi za vitabu. Kama tulivyoanza uumbaji wa mwanzo, tutaurudisha tena. Ni ahadi iliyo juu yetu. Hakika Sisi ni watendao.
105Na hakika tulikwishaandika katika Zaburi baada ya Kumbukumbu, ya kwamba ardhi watairithi waja wangu walio wema.
106Hakika katika haya yapo mawaidha kwa watu wafanyao ibada.
107Nasi hatukukutuma ila uwe ni rehema kwa walimwengu wote.
108Sema: Hakika imefunuliwa kwangu ya kwamba hakika Mungu wenu ni Mungu Mmoja tu. Je, Mmesilimu?
109Na kama wakigeuka, basi sema: Nimewatangazieni sawa sawa, wala sijui yako karibu au mbali hayo mliyoahidiwa.
110Hakika Yeye anajua kauli ya dhahiri na anajua myafichayo.
111Wala sijui pengine huu ni mtihani tu kwenu na starehe mpaka muda kidogo.
112Sema: Mola wangu Mlezi! Hukumu kwa haki. Na Mola wetu Mlezi ndiye Mwingi wa rehema, aombwaye msaada juu ya mnayoyazua.