ص
Sad • 88 ayahs • Meccan
بِسْمِ ٱللَّهِ ٱلرَّحْمَٰنِ ٱلرَّحِيمِ
1Swad. Ninaapa kwa Qur-ani yenye ukumbusho.[1]
2Lakini waliokufuru wamo katika majivuno na upinzani.
3Mataifa mangapi tumeyaangamiza kabla yao, na wakapiga kelele, lakini wakati wa kuokoka ulikwishapita.
4Na walistaajabu kuwajia mwonyaji anayetokana nao wenyewe, na makafiri wakasema: Huyu ni mchawi, mwongo mno.
5Amewafanya miungu wote kuwa ni mungu mmoja tu? Hakika hili ni jambo la ajabu.
6Na wakaondoka wakubwa wao wakiwaambia: Nendeni zenu na dumuni na miungu yenu, kwani hili ni jambo lililopangwa.
7Sisi hatukusikia haya katika mila hii ya mwisho. Haya si chochote ila ni uzushi tu.
8Ati yeye tu ndiye aliyeteremshiwa mawaidha peke yake katika sisi? Lakini hao wana shaka na mawaidha yangu, bali hawajaionja adhabu yangu.
9Au wanazo wao hazina za rehema za Mola wako Mlezi, Mwenye nguvu, Mpaji?
10Au wao wana ufalme wa mbingu na ardhi na vilivyo kati yavyo? Basi na wazipande njia za kwendea huko!
11Hao ni askari watakaoshindwa miongoni mwa makundi yatakayoshindwa.
12Walikanusha kabla yao kaumu ya Nuhu, na kina A'adi na Firauni mwenye majengo.
13Na Thamud na kaumu Luti na watu wa Machakani. Hayo ndiyo makundi.
14Hao wote waliwakadhibisha Mitume; basi wakastahiki adhabu yangu.
15Na hawa hawangojei ila ukelele mmoja tu usio wa kuchelewa.
16Na walisema: ‘Mola wetu Mlezi! Tuletee upesi sehemu yetu ya adhabu kabla ya Siku ya Hesabu.’
17Subiri kwa hayo wayasemayo, na umkumbuke mja wetu Daudi, mwenye nguvu. Hakika yeye alikuwa mwingi wa kutubia.
18Hakika tuliidhalilisha milima pamoja naye ikisabihi jioni na asubuhi pamoja naye.
19Na pia ndege waliokusanywa makundi kwa makundi; wote walikuwa wanyenyekevu kwake.
20Na tukautia nguvu ufalme wake, na tukampa hekima, na kukata hukumu.
21Na je, imekufikia habari ya wagombanao walipopindukia ukuta kuingia chumbani?
22Walipomuingilia Daudi, naye akawaogopa. Wakasema: Usiogope! Sisi ni wagombanao wawili, mmoja wetu amemdhulumu mwenziwe. Basi tuhukumu kwa haki, wala usipendelee. Na utuongoe kwenye njia iliyo sawa.
23Hakika huyu ndugu yangu ana kondoo wa kike tisini na tisa; na mimi ninaye kondoo mke mmoja. Akasema: Nipe huyo nikufugie! Na amenishinda kwa maneno.
24Akasema: Kweli amekudhulumu kwa kumtaka kondoo wako mmoja kuongezea kwenye kondoo wake. Na hakika washirika wengi hudhulumiana wao kwa wao, isipokuwa walioamini na wakatenda mema. Na hao ni wachache. Na Daudi akajua kuwa tumemfanyia mtihani. Basi akamwomba msamaha Mola wake Mlezi, na akaanguka kusujudu na kutubia.
25Basi tukamsamehe kwa hayo. Naye kwa hakika anao mkaribisho mkubwa na marejeo mazuri kwetu.
26Ewe Daudi! Hakika Sisi tumekufanya wewe uwe Khalifa katika nchi. Basi wahukumu watu kwa haki, wala usifuate matamanio yakakupoteza ambali na Njia ya Mwenyezi Mungu. Hakika wanaoipotea Njia ya Mwenyezi Mungu wakaiacha, watapata adhabu kali kwa sababu ya kusahau kwao Siku ya Hisabu.
27Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyo kati yake bure. Hiyo ni dhana ya waliokufuru. Ole wao waliokufuru kwa Moto utakaowapata.
28Je, tuwafanye walioamini na wakatenda mema kama wafanyao uharibifu katika nchi? Au tuwafanye wacha Mungu kama waovu?
29Na hiki Kitabu, tumekuteremshia wewe, kimebarikiwa, ili wazizingatie Aya zake, na wawaidhike wenye akili.
30Na Daudi tukamtunukia Suleiman. Alikuwa mja mwema. Na hakika alikuwa mwingi wa kutubia.
31Alipopelekewa jioni farasi wasimamao kidete, tayari kutoka shoti.
32Basi akasema: Navipenda vitu vizuri kwa kumkumbuka Mola wangu Mlezi. Kisha wakafichikana nyuma ya boma.
33(Akasema:) Nirudishieni hao! Basi akaanza kuwapapasa miguu na shingo.
34Na tulimtia mtihanini Suleiman, na tukauweka mwili juu ya kiti chake, kisha akarejea kwa kutubu.
35Akasema: Mola wangu Mlezi! Nisamehe na unipe ufalme usiomwelekea yeyote baada yangu. Hakika Wewe ndiye Mpaji.
36Basi tukaufanya upepo umtumikie, ukenda kwa amri yake, popote alipotaka kufika.
37Na tukayafanya mashetani yamtumikie, wote wajenzi na wapiga mbizi.
38Na wengine wafungwao kwa minyororo.
39Hiki ndicho kipawa chetu. Basi toa au zuia, bila ya hisabu.
40Na hakika yeye kwetu Sisi ana cheo cha kukaribishwa kwetu, na pahala pazuri pa kurejea.
41Na mkumbuke mja wetu Ayubu alipomwita Mola wake Mlezi akasema: Kwa hakika Shetani amenifikishia udhia na adhabu.
42(Akaambiwa:) Piga-piga ardhi kwa mguu wako! Basi haya maji baridi ya kuogea na ya kunywa.
43Na tukampa ahali zake na wengine kama wao pamoja nao, kuwa ni rehema itokayo kwetu, na iwe kumbusho kwa watu wenye akili.
44Na shika kicha cha vijiti tu mkononi mwako, kisha ndio upigie nacho, wala usivunje kiapo. Hakika tulimkuta mwenye subira, mbora wa waja, kwa hakika alikuwa mwingi wa kutubu.
45Na wakumbuke waja wetu, Ibrahim na Is-haqa na Yaa'qubu waliokuwa na nguvu na busara.
46Sisi tumewahusisha wao kwa sifa ya ukumbusho wa Akhera.
47Na hakika wao kwetu sisi ni wateuliwa walio bora.
48Na mtaje Ismail na Alyasaa na Dhulkifli, na wote hao ni katika walio bora.
49Huu ni ukumbusho. Na hakika wacha Mungu wana marudio mazuri.
50Bustani za milele zitakazofunguliwa milango yao kwa ajili yao.
51Humo wataegemea matakia, wawe wanaagiza humo matunda mengi na vinywaji.
52Na pamoja nao wake zao wenye kutuliza macho, hirimu moja.
53Haya ndiyo mliyoahidiwa kwa Siku ya Hisabu.
54Hakika hii ndiyo riziki yetu isiyomalizika.
55Ndiyo hivi! Na hakika wenye kuasi bila ya shaka watapata marudio maovu kabisa;
56Nayo ni Jahannamu! Wataingia humo. Nacho hicho ni kitanda kiovu mno cha kulalia.
57Ndiyo hivi! Basi na wayaonje maji ya moto na ya usaha!
58Na adhabu nyenginezo za namna hii.
59Hili ndilo kundi litakalo ingia pamoja nanyi. Hapana makaribisho mema kwao. Hakika hao wanaingia Motoni.
60Waseme: Lakini nyinyi! Hamna mapokezi mazuri! Nyinyi ndio mliotusababishia haya, napo ni pahala paovu kabisa!
61Waseme: Mola wetu Mlezi aliyetusababishia haya, mzidishie adhabu mara mbili Motoni.
62Watasema: Tuna nini hata hatuwaoni wale watu ambao tukiwahisabu ndio katika waovu?
63Tulikosea tulipowafanyia masihara, au macho yetu tu hayawaoni?
64Hakika hayo bila ya shaka ndiyo mahasimiano ya watu wa Motoni.
65Sema: Hakika mimi ni mwonyaji tu; na hapana mungu ila Mwenyezi Mungu Mmoja, Mtenda nguvu.
66Mola Mlezi wa mbingu na ardhi na vilivyo baina yake, Mwenye nguvu, Mwenye kusamehe.
67Sema: Hii ni habari kubwa kabisa.
68Ambayo nyinyi mnaipuuza.
69Sikuwa na elimu ya mambo ya viumbe wakuu watukufu walipokuwa wakishindana.
70Haikufunuliwa kwangu isipokuwa ya kwamba hakika mimi ni mwonyaji dhahiri.
71Mola wako Mlezi alipowaambia Malaika: Hakika Mimi nitaumba mtu kutokana na udongo.
72Na nitakapomkamilisha na kumpulizia roho inayotokana nami, basi muangukieni kwa kumtii.
73Basi wakasujudu Malaika wote pamoja.
74Isipokuwa Iblisi; alijivuna na akawa katika makafiri.
75Mwenyezi Mungu akamwambia: Ewe Iblisi! Kipi kilichokuzuia kumtii yule niliyemuumba kwa mikono yangu? Je, umejiona mkubwa, au umekuwa katika wakuu kweli?
76Akasema: Mimi ni bora kuliko yeye. Umeniumba kwa moto, na yeye umemuumba kwa udongo.
77Akasema: Basi toka humo, kwani hakika wewe umelaaniwa.
78Na hakika laana yangu itakuwa juu yako mpaka Siku ya Malipo.
79Akasema: Mola wangu Mlezi! Nipe muhula mpaka siku watakayofufuliwa viumbe.
80Mwenyezi Mungu akasema: Basi umekwisha kuwa miongoni mwa waliopewa muhula.
81Mpaka siku ya wakati maalumu.
82Akasema (Iblisi): Naapa kwa utukufu wako, bila ya shaka nitawapoteza wote.
83Isipokuwa wale waja wako miongoni mwao waliohitariwa.
84Akasema: Haki! Na haki ninaisema.
85Bila ya shaka nitaijaza Jahannamu kwa wewe na kwa hao wote wenye kukufuata miongoni mwao.
86Sema (Ewe Mtume): Sikuombeni ujira juu ya haya, wala mimi si katika wadanganyifu.
87Hayakuwa haya ila ni mawaidha kwa walimwengu wote.
88Na bila ya shaka mtajua habari zake baada ya muda.