النبأ
The Tidings • 40 ayahs • Meccan
بِسْمِ ٱللَّهِ ٱلرَّحْمَٰنِ ٱلرَّحِيمِ
1Wanaulizana kuhusu nini?
2Kuhusu Ile habari kuu.
3Ambayo kwayo wanahitalifiana.
4La! Karibu watakuja jua.
5Tena la! Karibu watakuja jua.
6Kwani hatukuifanya ardhi kama tandiko?
7Na milima kama vigingi?
8Na tukakuumbeni kwa jozi?
9Na tukakufanya kulala kwenu ni mapumziko?
10Na tukaufanya usiku ni nguo?
11Na tukaufanya mchana ni wa kuchumia maisha?
12Na tukajenga juu yenu saba zenye nguvu?
13Na tukaifanya taa yenye mwanga na joto.
14Na tukateremsha maji yanayoanguka kwa kasi kutoka mawinguni.
15Ili tutoe kwayo nafaka na mimea.
16Na mabustani yenye miti iliyokamatana.
17Hakika Siku ya uamuzi imewekewa wakati wake.
18Siku litakapopulizwa baragumu, nanyi mtakuja kwa makundi.
19Na mbingu zitafunguliwa, ziwe milango.
20Na milima itaondolewa na itakuwa kama sarabi.
21Hakika Jahannamu inangojea!
22Kwa walioasi ndio makazi yao.
23Wakae humo karne baada ya karne.
24Hawataonja humo chochote kibaridi wala kinywaji.
25Ila maji ya moto sana na usaha.
26Ndio malipo mwafaka.
27Hakika hao hawakuwa wakitaraji kuwa kuna hesabu (juu ya matendo yao).
28Na wakakanusha Aya zetu kwa nguvu.
29Na kila kitu Sisi tumekidhibiti kwa kukiandika.
30Basi onjeni! Nasi hatutakuzidishieni ila adhabu!
31Hakika wacha Mungu wanastahiki kufuzu.
32Mabustani na mizabibu.
33Na wake wazuri waliolingana nao.
34Na bilauri zilizojaa.
35Hawatasikia humo upuuzi wala uongo.
36Malipo kutoka kwa Mola wako Mlezi, kipawa cha kutosha.
37Mola Mlezi wa mbingu na ardhi na vilivyo baina yake, Arrahman (Mwingi wa rehema); hawamiliki usemi mbele yake!
38Siku atakaposimama Roho na Malaika kwa safu. Hawatasema ila yule ambaye Mwingi wa rehema atamruhusu, na atasema yaliyo sawa tu.
39Hiyo ndiyo Siku ya haki. Basi anayetaka, na ashike njia arejee kwa Mola wake Mlezi.
40Hakika tumekuhadharisheni adhabu iliyo karibu kufika; Siku ambayo mtu ataona yale yaliyotangulizwa na mikono yake; na kafiri atasema: Laiti ningelikuwa udongo!