الروم
The Romans • 60 ayahs • Meccan
بِسْمِ ٱللَّهِ ٱلرَّحْمَٰنِ ٱلرَّحِيمِ
1Alif Lam Mim.[1]
2Warumi wameshindwa.
3Katika nchi iliyo karibu. Nao baada ya kushindwa kwao watashinda.
4Katika miaka michache. Amri ni ya Mwenyezi Mungu kabla yake na baada yake. Na siku hiyo Waumini watafurahi.
5Kwa nusura ya Mwenyezi Mungu, humnusuru amtakaye. Naye ndiye Mwenye nguvu, Mwingi wa kurehemu.
6Ni ahadi ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu havunji ahadi yake. Lakini wengi wa watu hawajui.
7Wanajua hali ya dhahiri ya maisha ya dunia, na wameghafilika na Akhera.
8Je, hawajifikirii nafsi zao? Mwenyezi Mungu hakuumba mbingu na ardhi na vilivyo kati yake isipokuwa kwa Haki na kwa muda maalumu. Na hakika watu wengi bila ya shaka ni wenye kukufuru kuwa watakutana na Mola wao Mlezi.
9Je, hawatembei katika ardhi wakaona ulivyokuwa mwisho wa wale waliokuwa kabla yao? Nao walikuwa na nguvu zaidi kuliko wao, na wakaitimbua ardhi na wakaistawisha zaidi kuliko walivyoistawisha wao. Na Mitume wao wakawajia na ushahidi wa wazi. Basi hakuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwadhulumu, lakini wenyewe walikuwa wakijidhulumu nafsi zao.
10Kisha ulikuwa mwisho wa wale waliofanya ubaya ni mbaya zaidi kwa sababu walizikadhibisha Ishara za Mwenyezi Mungu, na wakawa wanazifanyia stihizai.
11Mwenyezi Mungu huanzisha uumbaji, tena akaurudisha mara ya pili, na kisha mtarejeshwa kwake.
12Na siku itakaposimama Saa ya Kiyama, wahalifu watakata tamaa.
13Wala hawatakuwa na waombezi wowote miongoni mwa wale waliokuwa wakiwashirikisha na Mwenyezi Mungu; na wao wenyewe watawakataa hao washirikishwa wao.
14Na siku itakaposimama Saa ya Kiyama, siku hiyo watatengana.
15Ama wale walioamini na wakatenda mema, watafurahishwa katika Bustani.
16Na ama wale waliokufuru na wakazikanusha Ishara zetu na mkutano wa Akhera, hao basi watahudhurishwa katika adhabu.
17Basi Subhanallah (Mtakaseni Mwenyezi Mungu) jioni na asubuhi.
18Na sifa zote njema ni zake katika mbingu na ardhi, na alasiri na adhuhuri.
19Hukitoa kilicho hai kutokana na kilichokufa, na hukitoa kilichokufa kutokana na kilicho hai. Na huihuisha ardhi baada ya kufa kwake. Na kama hivyo ndivyo mtavyofufuliwa."
20Na katika Ishara zake ni kuwa aliwaumba kwa udongo. Kisha mmekuwa watu mliotawanyika kote kote.
21Na katika Ishara zake ni kuwa aliwaumbia wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye ameweka mapenzi na rehema baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanaotafakari.
22Na katika Ishara zake ni kuumba mbingu na ardhi, na kutofautiana ndimi zenu na rangi zenu. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa wajuao.
23Na katika Ishara zake ni kulala kwenu usiku na mchana, na kutafuta kwenu fadhila zake. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanaosikia.
24Na katika Ishara zake huwaonyesha umeme kwa kuwatia hofu na tamaa. Na huwateremshia maji kutoka mbinguni, na kwa hayo huifufua ardhi baada ya kufa kwake. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa watu watumiao akili.
25Na katika Ishara zake ni kuwa mbingu na ardhi zimesimama kwa amri yake. Kisha atakapowaita mwito mmoja tu, hapo mtatoka kwenye ardhi.
26Na ni vyake Yeye vilivyo mbinguni na katika ardhi. Vyote vinamtii Yeye.
27Na Yeye ndiye anayeanzisha uumbaji, kisha ataurudisha mara nyingine. Na jambo hili ni jepesi zaidi kwake. Naye ndiye mwenye mfano bora zaidi katika mbingu na ardhi. Na Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
28Amewapigia mfano kutokana na nafsi zenu. Je, katika hao iliyowamiliki mikono yenu ya kulia mnao washirika katika hivyo tulivyowaruzuku, mkawa nyinyi katika hivyo ni sawasawa, mnawaogopa kama mnavyoogopana wenyewe kwa wenyewe? Namna hivyo tunazipambanua Aya zetu kwa watu watumiao akili.
29Bali waliodhulumu wamefuata mapendo ya nafsi zao pasina kujua. Basi ni nani atamwongoa ambaye Mwenyezi Mungu amempoteza? Wala hao hawatakuwa na wa kuwanusuru.
30Basi uelekeze uso wako sawasawa kwenye Dini kwa unyoofu, ndilo umbile la Mwenyezi Mungu alilowaumbia watu. Hapana mabadiliko katika uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo Dini iliyonyooka sawa. Lakini watu wengi hawajui.
31Muwe wenye kutubia kwake, na mcheni Yeye, na simamisheni Swala, na wala msiwe katika washirikina.
32Katika wale ambao kwamba wameigawanya dini yao, na wakawa makundi makundi, kila kikundi kinafurahia kilicho nacho.
33Na watu wanapoguswa na madhara, humwomba Mola wao Mlezi huku wanatubu kwake. Kisha akiwaonjesha rehema itokayo kwake, mara kikundi miongoni mwao humshirikisha Mola wao Mlezi.
34Kwa kuyakufuru yale tuliyowapa. Basi stareheni. Mtakuja jua!
35Au tumewateremshia hoja ambayo inazungumza juu ya kile walichokuwa wakishirikisha nacho?
36Na tunapowaonjesha watu rehema, huifurahia. Na ukiwasibu ubaya kwa iliyoyatanguliza mikono yao wenyewe, mara wanakata tamaa.
37Kwani hawaoni kwamba Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye na humkunjia amtakaye? Hakika katika hayo, zipo Ishara kwa watu wanaoamini.
38Basi mpe jamaa haki yake, na masikini, na msafiri. Hayo ni heri kwa wanaotaka uso wa Mwenyezi Mungu. Na hao ndio waliofaulu.
39Na mnachokitoa kwa riba ili kiongezeke katika mali ya watu, basi hakiongezeki mbele ya Mwenyezi Mungu. Lakini mnachokitoa kwa Zaka kwa kutaka uso wa Mwenyezi Mungu, basi hao ndio watakaozidishiwa.
40Mwenyezi Mungu ndiye aliyewaumba, kisha akawaruzuku, kisha atawafisha, na kisha atawafufua. Je, yupo yeyote katika hao mnaowashirikisha na Mwenyezi Mungu afanyae lolote katika hayo? Yeye ametakasika, na ametukuka mbali na hayo mnayomshirikisha naye.
41Uharibifu umedhihiri barani na baharini kwa yale iliyoyafanya mikono ya watu, ili Mwenyezi Mungu awaonjeshe baadhi ya yale waliyoyatenda. Huenda wakarejea kwa kutubu.
42Sema: Safirini duniani na muangalie ulikuwaje mwisho wa wale waliotangulia. Wengi wao walikuwa washirikina.
43Basi uelekeze uso wako sawasawa kwenye Dini iliyonyooka kabla ya kufika Siku hiyo isiyozuilika, inayotoka kwa Mwenyezi Mungu. Siku hiyo watu watatengana.
44Anayekufuru, basi ukafiri wake utakuwa juu yake mwenyewe. Na anayetenda mema, basi wanazitengenezea nafsi zao.
45Ili awalipe wale walioamini na wakatenda mema kutokana na fadhila yake. Hakika Yeye hawapendi makafiri.
46Na katika Ishara zake ni kuzituma pepo ziletazo bishara njema, na ili kuwaonjesha baadhi ya rehema zake, na ili majahazi yaende kwa amri yake; na mtafute kutokana na fadhila yake, na ili mumshukuru.
47Na hakika tulikwishawatuma Mitume kabla yako kwa kaumu zao, na wakawajia kwa hoja zilizo wazi. Tukawaadhibu wale waliofanya uhalifu. Na ilikuwa ni haki juu yetu kuwanusuru Waumini.
48Mwenyezi Mungu ndiye anayezituma pepo zikayatimua mawingu, kisha akayatandaza mbinguni kama apendavyo. Na akayafanya mapande mapande, basi ukaiona mvua inatoka ndani yake. Anapowafikishia awatakao katika waja wake, mara hao huwa na furaha.
49Na ingawa kabla ya kuteremshiwa walikuwa wenye kukata tamaa.
50Basi ziangalie athari za rehema ya Mwenyezi Mungu, jinsi anavyoihuisha ardhi baada ya kufa kwake. Basi hakika huyo ndiye bila ya shaka mwenye kuhuisha wafu. Na Yeye ni Muweza wa kila kitu.
51Na tungeutuma upepo na wakauona umekuwa rangi ya manjano, juu ya hayo wangeendelea kukufuru.
52Kwani wewe hakika huwafanyi maiti wakasikia, wala viziwi wakasikia wito wakishageuka kukupa mgongo.
53Wala wewe huwaongoi vipofu kutoka katika upotovu wao. Huwasikilizishi isipokuwa wale wanaoziamini Aya zetu. Hao ndio Waislamu, walionyenyekea.
54Mwenyezi Mungu ndiye aliyewaumba kutokana na udhaifu, kisha akajaalia nguvu baada ya unyonge, kisha akajaalia baada ya nguvu unyonge tena na ukongwe. Anaumba atakavyo. Naye ndiye ajuaye zaidi, Mwenye uweza wote.
55Na siku itakaposimama Saa ya Kiyama, wahalifu wataapa kwamba hawakukaa duniani isipokuwa saa moja tu. Hivyo ndivyo walivyokuwa wakipotoshwa.
56Na wale waliopewa elimu na Imani watasema: Hakika nyinyi mlikwishakaa katika hukumu ya Mwenyezi Mungu mpaka Siku ya kufufuliwa. Basi hii ndiyo Siku ya kufufuliwa! Lakini nyinyi mlikuwa hamuijui.
57Basi Siku hiyo hautawafaa wale waliodhulumu udhuru wao, wala haitatakiwa toba yao.
58Na hakika tulikwisha wapigia watu kila mfano katika hii Qur-ani. Na ukiwaletea Ishara yoyote, hapana shaka wale waliokufuru watasema, "Nyinyi si chochote isipokuwa ni wana batili."
59Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu anavyoziba kwenye nyoyo za wale wasiojua.
60Basi subiri. Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya haki. Wala kamwe wasikupaparishe hao wasiokuwa na yakini.