الشعراء
The Poets • 227 ayahs • Meccan
بِسْمِ ٱللَّهِ ٱلرَّحْمَٰنِ ٱلرَّحِيمِ
1Tw'a Siin Miim.[1]
2Hizi ni Aya za Kitabu kinachobainisha.
3Huenda ukaihiliki nafsi yako kwa kuwa hawawi Waumini.
4Tungependa, tungeliwateremshia kutoka mbinguni Ishara zikashinda zimezinyenyekea shingo zao.
5Wala hauwafikii ukumbusho mpya kutoka kwa Arrahman (Mwingi wa rehema), isipokuwa wao huupa mgongo.
6Kwa yakini wamekwishakanusha; kwa hivyo zitakuja wafikia habari za yale waliyokuwa wakiyafanyia stihizai.
7Je, hawakuiona ardhi, ni mimea mingapi tumeiotesha humo, ya kila namna nzuri?
8Hakika katika haya zipo Ishara. Lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini.
9Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Yeye Mwenye nguvu, Mwingi wa kurehemu.
10Na Mola wako Mlezi, alipomwita Musa, akamwambia: Nenda kwa kaumu madhalimu.
11Kaumu wa Firauni. Kwani hawamchi Mwenyezi Mungu?
12Akasema: Mola wangu Mlezi, hakika mimi ninachelea kwamba watanikadhibisha.
13Na kifua changu kina dhiki, na ulimi wangu haukunjuki vyema. Basi mtumie ujumbe Harun.
14Na wao wana dhambi niliyowafanyia, kwa hivyo ninahofu wanaweza kuniua.
15Akasema: Sivyo hivyo kabisa! Nendeni na miujiza yetu. Hakika Sisi tu pamoja nanyi, tunasikiliza.
16Basi nendeni kwa Firauni na mwambieni: Hakika sisi ni Mitume wa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
17Kwamba: Waachilie Wana wa Israili waende pamoja nasi.
18(Firauni) akasema: Je, sisi hatukukulea wewe utotoni, na ukakaa miongoni mwetu katika umri wako miaka mingi?
19Na ukatenda kitendo chako ulichotenda, nawe ukawa miongoni mwa wenye kukufuru?
20(Musa) akasema: Nilitenda hayo hapo nilipokuwa miongoni mwa wale waliopotea.
21Basi nikawakimbia nilipowahofu, tena Mola wangu Mlezi akanitunukia hukumu, na akanijaalia niwe miongoni mwa Mitume.
22Na hiyo ndiyo neema ya kunisimbulia, na wewe umewatia utumwani Wana wa Israili?
23Firauni akasema: Na ni nani huyo Mola Mlezi wa walimwengu wote?
24Akasema: Ndiye Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, na vilivyo baina yake, ikiwa nyinyi ni wenye yakini.
25(Firauni) akawaambia waliomzunguka: Kwani hamsikilizi?
26(Musa) akasema: Ndiye Mola wenu Mlezi, na Mola Mlezi wa baba zenu wa kwanza.
27(Firauni) akasema: Hakika huyu Mtume wenu aliyetumwa kwenu ni mwendawazimu.
28(Musa) akasema: Ndiye Mola Mlezi wa Mashariki na Magharibi na vilivyo baina yake, ikiwa nyinyi mnatia akilini.
29(Firauni) akasema: Ukijifanyia mungu mwingine asiyekuwa mimi, basi bila ya shaka nitakufunga gerezani.
30Akasema: Je, hata kama nitakuletea kitu cha kubainisha wazi?
31Akasema: Kilete basi, kama wewe ni katika wakweli.
32Basi akaitupa fimbo yake, mara ikawa nyoka wa kuonekana dhahiri.
33Na akautoa nje mkono wake, mara ukawa mweupe kwa watazamao.
34(Firauni) akawaambia waheshimiwa waliomzunguka: Hakika huyu ni mchawi mtaalamu.
35Anataka kuwatoa katika nchi yenu kwa uchawi wake. Basi mna shauri gani?
36Wakasema: Mpe muda yeye na kakaye na uwatume mijini wakusanyao watu.
37Wakuletee kila mchawi bingwa mtaalamu.
38Basi wakakusanywa wachawi kwa ajili ya miadi ya siku maalumu.
39Na watu wakaambiwa: Je, mtakusanyika?
40Huenda tutawafuata wachawi ikiwa wao ndio watakaoshinda.
41Basi walipokuja wachawi, wakamwambia Firauni: Je, tutapata ujira ikiwa sisi ndio tutakaoshinda?
42Akasema: Ndiyo! Na hakika mtakuwa katika watu wa mbele.
43Musa akawaambia: Tupeni mnavyotaka kutupa.
44Basi wakatupa kamba zao na fimbo zao, na wakasema: Kwa nguvu za Firauni hakika sisi hapana shaka ni wenye kushinda.
45Basi Musa akatupa fimbo yake, nayo mara ikavimeza vile walivyovizua.
46Hapo wachawi hao walipinduka wakasujudu.
47Wakasema: Tumemuamini Mola Mlezi wa walimwengu wote.
48Mola Mlezi wa Musa na Harun.
49(Firauni) akasema: Je, mmemuamini kabla ya kuwaruhusu? Bila ya shaka yeye basi ndiye mkubwa wenu aliyewafunza uchawi. Basi mtakuja jua! Nitakatakata mikono yenu na miguu yenu kwa kutofautisha. Na nitawasulubisha misalabani nyote.
50Wakasema: Haidhuru, kwani sisi ni wenye kurejea kwa Mola wetu Mlezi.
51Hakika sisi tunatumai kwamba Mola wetu Mlezi atatusamehe makosa yetu, kwa kuwa tumekuwa wa kwanza wa Waumini.
52Na tulimuamrisha Musa kwa ufunuo: Nenda na waja wangu wakati wa usiku. Kwa hakika mtafuatwa.
53Basi Firauni akawatuma mijini wakusanyaji.
54(Wakieneza): Hakika hawa ni kikundi kidogo.
55Nao kwa hakika wanatuudhi.
56Na sisi ni wengi, wenye kuchukua hadhari.
57Basi tukawatoa katika mabustani na chemchemi.
58Na mahazina, na vyeo vya heshima,
59Vivyo hivyo, na tukawarithisha hayo Wana wa Israili.
60Basi wakawafuata lilipochomoza jua.
61Na yalipoonana majeshi mawili haya, watu wa Musa wakasema: Hakika sisi bila ya shaka tumekutwa!
62(Musa) akasema: Hasha! Hakika yu pamoja nami Mola wangu Mlezi. Yeye ataniongoa!
63Na tulimletea Musa ufunuo tukamwambia: Piga bahari kwa fimbo yako. Basi ikatengana, na kila sehemu ikawa kama mlima mkubwa.
64Na tukawasongesha hapo karibu wale wengine.
65Tukawaokoa Musa na wale waliokuwa pamoja naye wote.
66Kisha tukawazamisha hao wengine.
67Hakika bila ya shaka katika hayo ipo Ishara; lakini wengi wao si wenye kuamini.
68Na kwa hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu, Mwingi wa kurehemu.
69Na wasomee habari za Ibrahim.
70Alipomwambia baba yake na kaumu yake: Mnaabudu nini?
71Wakasema: Tunaabudu masanamu, daima tunayanyenyekea.
72Akasema: Je, yanawasikia mnapoyaita?
73Au yanawafaa, au yanawadhuru?
74Wakasema: Bali tuliwakuta baba zetu wakifanya hivyo hivyo.
75Akasema: "Je, mmewaona hawa mnaowaabudu?
76Nyinyi na baba zenu wa zamani?
77Kwani hakika hao ni adui zangu, isipokuwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
78Ambaye ndiye aliyeniumba, na Yeye ndiye ananiongoa.
79Na ambaye ndiye ananilisha na kuninywesha.
80Na ninapougua, ni Yeye ndiye anayeniponesha.
81Na ambaye atanifisha, na kisha atanihuisha.
82Na ambaye ndiye ninayemtumai kunisamehe makosa yangu Siku ya Malipo.
83Mola wangu Mlezi! Nitunukie hukumu na uniunganishe na walio wema.
84Na unijalie nitajwe kwa wema na watu watakaokuja baadaye.
85Na unijalie katika warithi wa Bustani za neema.
86Na umsamehe baba yangu, kwani hakika alikuwa miongoni mwa wapotovu.
87Wala usinihizi Siku watakapofufuliwa.
88Siku ambayo kwamba mali haitafaa kitu wala wana.
89Isipokuwa mwenye kumjia Mwenyezi Mungu na moyo safi."
90Na Bustani ya mbiguni itasogezwa kwa wacha Mungu.
91Na Jahannamu itadhihirishwa kwa wapotovu.
92Na wataambiwa: Wako wapi mliokuwa mkiwaabudu.
93Badala ya Mwenyezi Mungu? Je, wanawasaidia, au wanajisaidia wenyewe?
94Basi watavurumizwa humo wao na hao wakosefu.
95Na majeshi ya Ibilisi yote.
96Watasema, na hali ya kuwa wanazozana humo:
97"Tallahi! Kwa yakini tulikuwa katika upotovu ulio dhahiri.
98Tulipowafanya nyinyi ni sawa na Mola Mlezi wa walimwengu wote.
99Na hawakutupoteza isipokuwa wale wakosefu.
100Basi hatuna waombezi wowote.
101Wala rafiki wa dhati.
102Laiti tungelipata kurejea tena, tungelikuwa katika Waumini."
103Hakika katika haya ipo Ishara, lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini.
104Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwingi wa kurehemu.
105Kaumu ya Nuhu waliwakadhibisha Mitume.
106Alipowaambia ndugu yao, Nuhu: Je, hamumchi Mwenyezi Mungu?
107Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu.
108Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nitiini mimi.
109Na siwaulizi juu yake ujira, kwani ujira wangu hauko isipokuwa kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
110Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nitiini mimi.
111Wakasema: Je, tukuamini wewe, ilhali wanaokufuata ni watu duni?
112Akasema: Ninayajuaje waliyokuwa wakiyafanya?
113Hesabu yao haiko isipokuwa kwa Mola wao Mlezi, laiti mngelitambua!
114Wala mimi si wa kuwafukuza Waumini.
115Mimi si chochote isipokuwa ni Mwonyaji wa dhahiri shahiri.
116Wakasema: Ikiwa huachi, ewe Nuhu, bila ya shaka utapigwa mawe.
117Akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika watu wangu wamenikadhibisha.
118Basi hukumu baina yangu na wao kwa hukumu yako, na uniokoe mimi na walio pamoja nami miongoni mwa Waumini.
119Kwa hivyo tukamwokoa yeye na waliokuwa pamoja naye katika marikebu iliyosheheni.
120Kisha tukawazamisha baadaye waliobakia.
121Hakika katika haya ipo Ishara, lakini si wengi wao waliokuwa Waumini.
122Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Yeye Mwenye nguvu, Mwingi wa kurehemu.
123Kina 'Aad waliwakanusha Mitume.
124Alipowaambia ndugu yao, Hud: Je, hamumchi Mungu?
125Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu.
126Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nitiini mimi.
127Wala siwaulizi juu yake ujira wowote, kwani ujira wangu hauko isipokuwa kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
128Je, mnajenga juu ya kila mnyanyuko kumbusho la kufanyia upuuzi?
129Na mnajenga majengo ya kifahari kama kwamba mtaishi milele!
130Na mnapotumia nguvu, mnatumia nguvu kwa ujabari.
131Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nitiini.
132Na mcheni aliyewapa haya mnayoyajua.
133Aliwapa wanyama wa kufuga na wana.
134Na mabustani na chemchemi.
135Hakika mimi ninawahofia adhabu ya Siku Kubwa.
136Wakasema: Ni mamoja kwetu, ukitupa mawaidha au hukuwa miongoni mwa watoao mawaidha.
137Haya si chochote isipokuwa ni mtindo wa watu wa tokea zamani.
138Wala sisi hatutaadhibiwa.
139Wakamkadhibisha; nasi tukawaangamiza. Hakika bila ya shaka katika haya ipo Ishara. Lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini.
140Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu, Mwingi wa kurehemu.
141Kina Thamud waliwakadhibisha Mitume.
142Alipowaambia ndugu yao Saleh: Je, hamumchi Mungu?
143Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu.
144Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nitiini.
145Wala siwaulizi ujira wowote juu yake. Ujira wangu hauko isipokuwa kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
146Je, mtaachwa salama salimini katika haya yaliyopo hapa?
147Katika mabustani, na chemchemi?
148Na konde na mitende yenye makole yaliyowiva.
149Na mnachonga milimani majumba kwa ustadi.
150Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nitiini mimi.
151Wala msitii amri za waliopitiliza mipaka.
152Ambao wanafanya uharibifu katika nchi, wala hawatengenezi.
153Wakasema: Hakika wewe ni miongoni mwa waliorogwa.
154Wewe si chochote isipokuwa ni mtu kama sisi. Basi leta Ishara ikiwa wewe ni miongoni mwa wakweli.
155Akasema: Huyu ngamia jike; awe na zamu yake ya kunywa, na nyinyi muwe na zamu yenu ya kunywa katika siku maalumu.
156Wala msimguse kwa wovu, ikawashika adhabu ya Siku Kubwa.
157Lakini wakamuua, na wakawa wenye kujuta.
158Basi ikawapata adhabu. Hakika katika hayo ipo Ishara. Lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini.
159Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu, Mwingi wa kurehemu.
160Watu wa Luti waliwakadhibisha Mitume.
161Alipowaambia ndugu yao, Luti: Je, hamumchi Mungu?
162Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu.
163Basi mcheni Mwenyezi Mungu na nitiini mimi.
164Wala mimi sikuwauliza ujira wowote juu yake; ujira wangu hauko isipokuwa kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
165Je, katika viumbe vyote mnawaingilia wanaume?
166Na mnaacha alichowaumbia Mola wenu Mlezi katika wake zenu? Ama kweli nyinyi ni watu mnaoruka mipaka!
167Wakasema: Ewe Luti! Usipoacha, hapana shaka utakuwa miongoni mwa wanaotolewa mji!
168Akasema: Hakika mimi ni katika wanaokichukia hiki kitendo chenu.
169Mola wangu Mlezi! Niokoe mimi na ahali zangu na haya wayatendayo.
170Basi tukamwokoa yeye na ahali zake wote.
171Isipokuwa kikongwe katika waliokaa nyuma.
172Kisha tukawaangamiza wale wengine.
173Na tukawanyeshea mvua, basi ni ovu mno mvua ya waliyoonywa.
174Hakika katika hayo ipo Ishara. Na hawakuwa wengi wao wenye kuamini.
175Na hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka ndiye Mwenye nguvu, Mwingi wa kurehemu.
176Watu wa Machakani waliwakanusha Mitume.
177Shuaibu alipowaambia: Je, hamumchi Mungu?
178Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu.
179Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nitiini mimi.
180Wala siwaulizi ujira wowote juu yake. Ujira wangu hauko isipokuwa kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
181Timizeni kipimo sawasawa, wala msiwe katika wanaopunja.
182Na pimeni kwa haki iliyonyooka.
183Wala msiwapunje watu vitu vyao, wala msifanye jeuri katika ardhi kwa kufanya uharibifu.
184Na mcheni aliyewaumba nyinyi na vizazi vilivyotangulia.
185Wakasema: Hakika wewe ni katika waliorogwa.
186Na wewe si chochote isipokuwa ni mtu tu kama sisi, na kwa yakini tunakuona wewe ni katika waongo.
187Hebu tuangushie vipande kutoka mbinguni ikiwa wewe ni miongoni mwa wakweli.
188Akasema: Mola wangu Mlezi anajua zaidi mnayoyatenda.
189Basi walimkanusha, na ikawashika adhabu ya Siku ya kivuli. Hakika hiyo ilikuwa adhabu ya Siku kubwa.
190Hakika katika hayo ipo Ishara, lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini.
191Na hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka ndiye Yeye Mwenye nguvu, Mwingi wa kurehemu.
192Na bila ya shaka hii ni Uteremsho wa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
193Ameuteremsha Roho muaminifu.
194Juu ya moyo wako, ili uwe katika Waonyaji.
195Kwa ulimi wa Kiarabu ulio wazi.
196Na hakika bila ya shaka haya yamo katika Vitabu vya kale.
197Je, haikuwa kwao ni Ishara kwamba wanayajua haya wanachuoni wa Wana wa Israili?
198Na lau kuwa tungeliiteremsha juu ya mmoja wa wasiokuwa Waarabu.
199Na akawasomea, wasingelikuwa wenye kuamini.
200Namna hivi tunaingiza katika nyoyo za wahalifu.
201Hawataiamini mpaka waione adhabu chungu.
202Basi itawafikia kwa ghafla, na hali hawana habari.
203Na watasema: "Je, tutapewa muhula?"
204Basi je, wanaihimiza adhabu yetu?
205Waonaje kama tukiwastarehesha kwa miaka.
206Kisha yakawafikia waliyokuwa wakiahidiwa.
207Yatawafaa nini yale waliyostareheshewa?
208Wala hatukuangamiza mji wowote isipokuwa ulikuwa na waonyaji.
209Kuwa ni ukumbusho. Wala Sisi hatukuwa wenye kudhulumu.
210Wala Mashetani hawakuteremka nayo.
211Wala haitakiwi kwao, na wala hawawezi.
212Hakika hao wametengwa na kusikia.
213Basi usimwombe mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu ukawa miongoni mwa watakaoadhibiwa.
214Na uwaonye jamaa zako walio karibu nawe.
215Na watwae kwa upole wanaokufuata miongoni mwa Waumini.
216Na ikiwa watakuasi, basi sema: Mimi ninajitenga mbali na hayo mnayoyatenda.
217Na umtegemee Mtukufu Mwenye nguvu, Mwingi wa kurehemu.
218Ambaye anakuona unaposimama.
219Na mageuko yako katika wanaosujudu.
220Hakika Yeye ndiye Mwenye kusikia, Mwenye kujua zaidi.
221Je, niwaambieni nani wanawashukia Mashetani?
222Wanamshukia kila mzushi mkubwa mwingi wa dhambi.
223Wanawapelekea yale wanayoyasikia; na wengi wao ni waongo.
224Na watungaji mashairi ni wapotovu ndio wanawafuata.
225Je, huwaoni kwamba wao wanatangatanga katika kila bonde?
226Na kwamba wao husema wasiyoyatenda?
227Isipokuwa wale walioamini, na wakatenda mema, na wakamkumbuka Mwenyezi Mungu kwa wingi, na wakajitetea wanapodhulumiwa. Na wanaodhulumu watakuja jua mgeuko gani watakaogeuka.