محمد
Muhammad • 38 ayahs • Medinan
بِسْمِ ٱللَّهِ ٱلرَّحْمَٰنِ ٱلرَّحِيمِ
1Wale waliokufuru na wakazuilia njia ya Mwenyezi Mungu, Yeye atavipotoa vitendo vyao.
2Na wale walioamini, na wakatenda mema, na wakaamini yale aliyoteremshiwa Muhammad - nayo ni Haki iliyotoka kwa Mola wao Mlezi - atawafutia makosa yao na ataitengeneza hali yao.
3Hayo ni kwa sababu wale waliokufuru wamefuata upotovu, na wale walioamini wamefuata Haki iliyotoka kwa Mola wao Mlezi. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyowapigia watu mifano yao.
4Basi mnapowakuta wale waliokufuru, wapigeni shingoni mwao, mpaka mkiwadhoofisha, wafungeni pingu. Tena waachilieni kwa hisani au wajikomboe, mpaka vita vipoe. Ndivyo hivyo. Na lau angelitaka Mwenyezi Mungu, angeliwashinda mwenyewe, lakini haya ni kwa sababu awatie mitihani nyinyi kwa nyinyi. Na wale waliouliwa katika njia ya Mwenyezi Mungu, hatayapoteza matendo yao.
5Atawaongoza na awatengezee hali yao.
6Na atawaingiza katika Pepo aliyowajuulisha.
7Enyi mlioamini! Mkimnusuru Mwenyezi Mungu, naye atakunusuruni na ataiimarisha miguu yenu.
8Na wale waliokufuru, basi kwao ni maangamizo, na atavipoteza vitendo vyao.
9Hayo ni kwa sababu waliyachukia yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, basi akaviangusha vitendo vyao.
10Kwani hawakutembea katika ardhi wakaona ulikuwaje mwisho wa wale waliokuwa kabla yao? Mwenyezi Mungu aliwaangamiza, na kwa makafiri hawa itakuwa mifano ya hayo.
11Hayo ni kwa sababu Mwenyezi Mungu ni Mlinzi wa wale walioamini. Na makafiri hawana mlinzi.
12Hakika Mwenyezi Mungu atawaingiza wale walioamini na wakatenda mema katika Bustani za mbinguni zipitiwazo na mito kati yake. Na wale waliokufuru hujifurahisha na hula kama walavyo wanyama, na Moto ndio makazi yao.
13Na ni miji mingapi iliyokuwa na nguvu zaidi kuliko mji wako huu uliokutoa? Tuliwateketeza na wala hawakuwa na yeyote wa kuwanusuru.
14Je, yule aliye kwenye ubainifu kutoka kwa Mola wake Mlezi ni kama yule aliyepambiwa uovu wa vitendo vyake, na wakafuata matamanio yao?
15Mfano wa Bustani ya mbinguni waliyoahidiwa wacha Mungu, ina mito ya maji yasiyovunda, na mito ya maziwa yasiyoharibika ladha yake, na mito ya mvinyo wenye ladha kwa wanywao, na mito ya asali iliyosafishwa. Na wao humo watakuwa na kila namna ya matunda, na maghfira kutoka kwa Mola wao Mlezi. Basi hao ni kama watakaodumu Motoni na wakinyweshwa maji yanayochemka ya kuwakatakata matumbo yao?
16Na wapo miongoni mwao wanaokusikiliza, mpaka wakiondoka kwako, huwauliza waliopewa elimu: 'Amesema nini sasa hivi?' Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu ameziba nyoyo zao, na wakafuata matamanio yao.
17Na wale walioongoka anawazidishia uongofu na anawapa ucha Mungu wao.
18Kwani wanangojea jengine isipokuwa iwafikie Saa (ya Kiyama) kwa ghafla? Na hakika alama zake zimekwisha kuja. Na itakapowajia, kutawafaa nini kukumbuka kwao?
19Basi jua ya kwamba hapana mungu ila Mwenyezi Mungu, na omba maghufira kwa dhambi zako na za Waumini wanaume na Waumini wanawake. Na Mwenyezi Mungu anajua mahali penu pa kwenda na kurudi, na mahali penu pa kukaa.
20Na Waumini wanasema: 'Kwa nini haiteremshwi Sura?' Na inapoteremshwa Sura madhubuti na ikatajwa ndani yake habari ya vita, utawaona wenye maradhi katika nyoyo zao wanakutazama mtazamo wa anayezimia kwa sababu ya mauti. Basi ni bora kwao.
21Utiifu na kauli njema. Na jambo likishaazimiwa, basi wakiwa ni wakweli kwa Mwenyezi Mungu, bila ya shaka itakuwa ni heri kwao.
22Basi mnatarajia kwamba mkigeuka mkaenda zenu kwamba ndio mtafanya uharibifu katika nchi na muwatupe jamaa zenu?
23Hao ndio aliowalaani Mwenyezi Mungu, na akawatia uziwi, na akawapofua macho yao.
24Je, hawaizingatii hii Qur-ani? Au kwenye nyoyo (zao) zipo kufuli zake?
25Kwa hakika wale wanaorudi nyuma baada ya uongofu kwisha wabainikia, Shetani huyo amewashawishi na amewaghuri.
26Hayo ni kwa sababu waliwaambia wale waliochukia yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu: 'Tutakutiini katika baadhi ya mambo.' Na Mwenyezi Mungu anajua siri zao.
27Basi itakuwaje Malaika watakapowafisha wakawa wanawapiga nyuso zao na migongo yao!
28Hayo ni kwa sababu wao waliyafuata yale yaliyomchukiza Mwenyezi Mungu na wakachukia yanayomridhisha, basi akaviangusha vitendo vyao.
29Je, wenye maradhi nyoyoni mwao wanadhani kwamba Mwenyezi Mungu hatazidhihirisha chuki zao?
30Na tungelipenda, tungelikuonyesha hao na ungeliwatambua kwa alama zao. Lakini bila ya shaka utawajua kwa namna ya msemo wao. Na Mwenyezi Mungu anavijua vitendo vyenu.
31Na bila ya shaka tutawajaribu mpaka tuwajue wapiganao Jihadi katika nyinyi na wanaosubiri. Nasi tutazifanyia mtihani habari zenu.
32Kwa hakika wale waliokufuru na wakazuilia njia ya Mwenyezi Mungu na wakapingana na Mtume baada ya uongofu kwisha wabainikia, hao hawatamdhuru Mwenyezi Mungu kwa lolote. Naye ataviangusha vitendo vyao.
33Enyi mlioamini! Mtiini Mwenyezi Mungu, na mtiini Mtume, wala msiviharibu vitendo vyenu.
34Hakika wale waliokufuru na wakazuilia njia ya Mwenyezi Mungu, kisha wakafa na hali ni makafiri, Mwenyezi Mungu hatawasamehe makosa yao.
35Basi msilegee na mkataka suluhu, maana nyinyi ndio mtakaoshinda. Na Mwenyezi Mungu yu pamoja nanyi, wala hatawanyima malipo ya vitendo vyenu.
36Hakika uhai wa duniani ni mchezo na pumbao. Na mkiamini na mkamcha Mungu, Mwenyezi Mungu atakupeni ujira wenu, wala hatakutakeni mali zenu.
37Na akikutakeni hizo na kukushikilieni, mtafanya ubahili, na atatoa undani wa chuki zenu.
38Angalieni! Nyinyi hawa mnaitwa mtumie mali katika njia ya Mwenyezi Mungu, na wapo katika nyinyi wanaofanya ubahili. Na anayefanya ubahili, basi anajifanyia ubahili mwenyewe. Na Mwenyezi Mungu si mhitaji, na nyinyi ndio wahitaji. Na mkigeuka, atawaleta watu wengine badala yenu, nao hawatakuwa kama nyinyi.